Mwenge wa Olimpiki wawasili Rio de Janeiro,Brazil

Mwenge wa Olimpiki wawasili Brazil baada ya safari ya miezi mitatu ndani ya Brazil yenyewe. Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mwenge wa Olimpiki watua Rio Janeiro

Mwenge wa Olimpiki umefika katika mji wa Rio de Janeiro kwa kutumia usafiri wa boti baada ya ziara ya muda wa miezi mitatu kuzunguuka miji mikubwa ya Brazil.

Meya wa mji wa Rio, Eduardo Paes, ndiye aliyeubeba mwenge huo wa Olimpiki miongoni mwa watu wachache waliofanikiwa kuushika.

Safari hiyo ya miezi mitatu haikuwa rahisi kwani kuna wakati msafara wa mwenge huo wa Olimpiki ulipokuwa ukipitishwa ulikumbana na waandamanaji wenye hasira kali kuhusiana na suala la gharama kubwa zilizotumika mpaka kuwa wenyeji wa michuano hiyo maarufu ulimwenguni.

Polisi wa kutuliza ghasia iliwalazimu kutumia mabomu ya machozi na pilipili za kupuliza ili kuwatawanya waandamanaji hao wenye hasira .Kwa sasa nchi ya Brazil inapita katika kipindi cha mpito wa hali mbaya ni katika mtego wa anguko kubwa la kiutawala na mgogoro wa kisiasa, na maandamano zaidi yanatarajiwa siku ya ufunguzi wa michuano hiyo ya Olimpiki inayotarajiwa siku ya Ijumaa.

Waandaaji wa michuano hiyo wameonesha masikitiko yao makubwa kutokana na mwitikio mdogo ulooneshwa na wabrazil kwani tiketi zaidi ya milioni moja bado hazijanunuliwa huku sherehe za ufunguzi zimekaribia.