Jubaland yasitisha mpango wa kuwapokea wakimbizi

Rais wa jimbo la Jubaland nchini Somalia
Image caption Rais wa jimbo la Jubaland nchini Somalia Ahmed Madobe

Mamlaka katika jimbo la Jubaland nchini Somalia imetangaza kusitisha shughuli ya kuwapokea wakimbizi wa Somalia wanaowasili katika eneo hilo kutoka Kenya.

Shughuli ya kuwarudisha makwao wakimbizi hao kutoka kambi ya Dadaab ilianza mwaka 2014,lakini imeongeza kasi mwaka huu baada ya Kenya kutangaza kuwa inafunga kambi kubwa ya wakimbizi ya Dadaab.

Waziri wa maswala ya ndani katika jimbo la Juba Mohammed Warsame Darwish ameambia BBC kwamba wakimbizi hao wanakabiliwa na hatari zaidi kwa sababu hawapati misaada ya kibinaadamu ilioahidiwa kwao wakati watakapowasili katika maeneo yanayodhibitiwa.

Waziri huyo amelaumu shirika la wakimbizi katika Umoja wa mataifa UNHCR kwa kutofuata mipango iliowekwa na badala yake limekuwa likiwawacha wakimbizi hao katika maeneo yanayodhibitiwa na mamlaka ya jimbo hilo.