Homa ya Ndege yagunduliwa Uganda

Aina ya Bata wa kufugwa ambao wanaaminika kuambukizwa homa ya Ndege Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bata wa kufugwa ni miongoni mwa ndege wanaoweza kuambukizwa homa hiyo.

Serikali ya Uganda, imethibitisha kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya ndege katika maeneo karibu na fuo za Ziwa Victoria.

Virusi hivyo vimegunduliwa katika ndege wa porini wanaohama hama, bata wanaofugwa na kuku.

Wakuu sasa wametoa tahadhari kwa jamii za maeneo hayo kuhakikisha kuwa ugonjwa huo hausambai na kuwaambukiza watu.

Mwaandishi wa BBC nchini Uganda, Catherine Byaruhanga anasema kuwa ripoti za awali za ndege waliokufa zilianza kutolewa mwanzo tu wa mwaka huu.

Wakazi wa maeneo hayo, wamesema kuwa, walipata mizoga ya ndege wengi waliokuwa wakihamia Uganda wakati wa majira ya baridi kutoka maeneo ya kaskazini mwa dunia.

Uchunguzi uliofanywa na wataalamu, yalithibitisha kuwa ndege hao walifariki kutokana na maradhi ya Highly Pathogenic Avian Influenza au bird flu, yaani homa kali ya ndege kama inavyofahamika.

Chembechembe zilizokusanywa kutoka kwa mizoga ya bata wa kufugwa na kuku, katika Wilaya moja ya eneo hilo karibu na Ziwa Victoria upande wa Uganda, zilithibitisha hilo.

Hakuna taarifa zozote za ugonjwa huo kuambukiza binadamu zilizotolewa kufikia sasa, na serikali ya Uganda imesema kuwa inawashauri wakazi wa maeneo hayo kuhusu namna ya kujikinga kupatwa na ugonjwa huo na mbinu za kuzuia kusambaa zaidi.

Vikosi vya majanga ya dharura vimetumwa huko ili kukusanya mizoga ya ndege hao waliokufa.

Hii ni mara ya kwanza kwa mlipuko wa ugonjwa huo kutokea nchini Uganda, lakini mamlaka kuu ya nchi hiyo, imefumbua mbinu mpya ya kukabiliana kwa haraka namna ya kushughulikia majanga ya dharura ya kiafya, hasa kufuatia visa vya ugonjwa hatari wa Ebola.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii