Magari ya Ford aina ya Kugas, Afrika Kusini yarejeshwa kutokana na kuwaka moto

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Magari yanayorejeshwa yaliundiwa Uhispania

Kampuni ya kuunda magari ya Ford Afrika Kusini, yarejesha magari aina ya Kugas kwa sababu ya kuwaka moto

Kampuni kubwa ya kuunda magari ya Ford imeanza kurejesha magari 4,500 aina ya Kuga nchini Afrika Kusini kwa sababu ya kiusalama, baada ya zaidi ya magari 50 kushika moto tangu mwaka 2015.

Mkurugenzi mkuu wa Ford, Afrika Kusini Jeff Nemeth amesema kuwa uchunguzi unaonyesha kuwa kutokea kwa moto, kulisababishwa na muongezeko wa joto kwenye injini yake na kusababisha kuvuja kwa mafuta.

Bwana Nemeth alisema hayo katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari kwa pamoja na tume ya wamiliki na waundaji bidhaa ya Taifa hilo- NCC, ambayo imekuwa ikishinikiza kampuni hiyo ya magari kuchukua hatua. "Swala hili limejikokota kwa muda mrefu," amesema kamishena mkuu wa tume hiyo Ibrahim Mohammad.

Magari yanayorejeshwa ni yenye muundo wa uwezo wa kubeba mafuta lita 1.6 iliyojengewa Uhispania kati ya mwaka 2012 na 2014.

Kampuni hiyo imo kwenye shinikizo kubwa kuchukua hatua tangu mwendesha gari mmoja Reshell Jimmy, 33, alipoteketea hadi kufa ndani ya gari muundo wa Kuga mwaka 2015.

Jumla ya magari 48 yameteketea nchini Afrika Kusini, 11 kati yao mwezi huu pekee. Hayo yameripotiwa na gazeti moja la nchi hiyo TimesLive.