Mabeyo aapishwa kuwa mkuu mpya wa Jeshi, Tanzania

Rais Magufuli amkaribisha Ikulu Jenerali Venance Mabeyo Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais Magufuli amkaribisha Ikulu Jenerali Venance Mabeyo

Rais John Pombe Magufuli, amemuapisha mkuu mpya wa majeshi ya ulinzi nchini Tanzania Jenerali Venance Mabeyo.

Sherehe za kuapishwa zilifanyika katika Ikulu ya Rais iliyoko katika mji mkuu Dar es Salaam.

Jenerali Mabeyo aliteuliwa juma lililopita kuchukua mahala pa Jenerali Davis Mwamunyange ambaye amestaafu.

Kabla ya kuteuliwa kwake, Bwana Mabeyo alikuwa mmoja wa maafisa wakuu katika jeshi la Tanzania (TPDF), kabla ya kufanywa rasmi kuwa jenerali.

Jenerali Mabeyo amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Jenerali Davis Mwamunyange ambaye amestaafu.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amemuapisha Maja Jenerali James Mwakibolwa, ambaye sasa anasimamia rasmi jeshi la Tanzania, kuchukua nafasi iliyoachwa na Jenerali Mabeyo.

Halikadhalika, Mheshimiwa. Rais Magufuli amemuapisha Mhe. Balozi. Luteni Jenerali Mstaafu Paul Meela kuwa Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).Mheshimiwa Balozi Luteni Jenerali Mstaafu Paul Meela, anachukua nafasi ya Mheshimiwa Balozi Antony Ngereza Cheche ambaye amestaafu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia tukio la kuapishwa kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kamishna Robert Boazi Mikomangwa.

Dkt. Magufuli ametoa wito kwa uongozi mpya wa Jeshi chini ya Jenerali Venance Mabeyo, kuendeleza juhudi za kuilinda nchi na pia ametaka majeshi yote nchini Tanzania yajipange kuendana na sera ya ujenzi wa viwanda, kwa kuhakikisha viwanda vya kutengeneza mahitaji yanayoweza kupatikana nchini humo kwa ajili ya majeshi kama vile sare na vifaa, vinajengwa.