Man City haina nia ya kumuuza Sergio Aguero

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Sergio Aguero amefungia Manchester City jumla ya mabao 18 msimu huu

Timu ya Manchester City, haina nia ya kumuuza Sergio Aguero msimu huu wa kiangazi, licha ya mshambulizi huyo kuachwa nje ya timu katika mechi mbili zilizopita.

Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 28 alitia saini kuongeza kandarasi yake msimu huu, ikiwa na maana kuwa anasalia na miaka mitatu katika mapatano hayo.

Baada ya kutoka benji pale City ilippopata ushindi wa 2-1 dhidi ya Swansea, Aguero amesema kuwa: "Bila shaka siondoki, nataka kusalia.

"Katika hili, kwa miezi mitatu ijayo inafaa niisaidie klabu na hapo wataamua kama nina nafasi au la."

Licha ya Aguero, kutarajia uamuzi kufanywa msimu huu wa kiangazi, viongozi wakuu wa Man City, waliashiria siku ya Jumapili kwamba, hawana nia ya kumuuza mchezaji huyo.

Mchezaji huyo wa mbele wa timu ya Argentina, alicheza dakika saba za mwisho, pale Manchester City ilipojipatia ushindi dhidi ya Swansea, baada ya Gabriel Jesus kujeruhiwa, mechi ya pili kwa mbrazil huyo, aliyechukua mahala pa Aguero katika kikosi cha kwanza cha wachezaji 11.