James Oswago wa IEBC zamani Kenya, akamatwa

Haki miliki ya picha AP
Image caption Afisa wa Tume ya uchaguzi chini Kenya akisawazisha matokeo ya kura

Aliyekuwa afisa mkuu mtendaji wa tume ya uchaguzi nchini Kenya, amekamatwa na kufikishwa mahakamani Jumatano kwa tuhuma ya kuhusika na ufisadi.

James Oswago na wengine watatu, wanashutumiwa kwa kuchukua mlungula kutoka kwa kampuni moja ya Uingereza inayojihusisha na uchapishaji, iliyopewa kandarasi ya kuchapisha makaratasi pamoja na masanduku ya kupigia kura, katika uchaguzi mkuu uliopita nchini humo.

Wamekanusha mashtaka dhidi yao.

Kashfa hiyo kubwa iliyohusisha kupotea kwa mamilioni ya dola ilipewa jina "chickengate" na vyombo vya habari nchini Kenya.

Kashfa hiyo ilifichuliwa baada ya mahakama jijini London iliwashtaki na kuwafunga jela wakurugenzi wakuu wa kampuni moja ya uchapishaji nchini Uingereza Smith and Ouzman, kwa kuwapa hongo maafisa hao wa Kenya zaidi ya dola 374,000, ili kupewa kandarasi ya uchapishaji wa makaratasi ya mtihani na ya kupigia kura kati ya mwaka 2008 na 2010.

Inadaiwwa kuwa Bwana Oswago, ambaye alikuwa afisa mkuu mtendani wa tume hiyo wakati huo, alifanya kazi kwa karibu mno na wakala Trevy Oyombra, ambaye pia amekamatwa, ili kuongeza bei ya kufanya kazi hiyo na kuficha hongo hiyo.

Hongo hiyo ilipewa jina "chicken".

Mnamo mwaka 2016, afisa mmoja wa Uingereza anayekabiliana na ufisadi alizitoa barua pepe za mawasiliano, stakabadhi za kusafirisha kwa meli makaratasi hayo na risiti za ununuzi, kama ushahidi katika kesi hiyo huko Uingereza hadi kwa muendesha mashtaka nchini Kenya, aliyeanzisha uchunguzi.

Watu hao wote watatu wameachiliwa kwa dhamana.