Afcon 2017: Caf yaapa kuboresha viwanja vya soka

Haki miliki ya picha JUSTIN TALLIS
Image caption Uwanja wa Michezo wa Port-Gentil, ulikosolewa pakubwa

Shirikisho la kandanda Barani Afrika (Caf), linasema kwamba litaamua kuchukua udhibiti wa kuviboresha viwanja vya soka, vitakavyotumika siku zijazo kusakatia dimba la kombe la mataifa bingwa barani humo, ili kuepusha viwanja vibofu.

Viwanja vilivyotumika kwa mashindano hayo mwaka huu huko Gabon, vimekosolewa pakubwa, huku mkufunzi wa timu ya taifa ya Ghana Avram Grant, akilalamikia hali mbovu ya zulia kwenye uwanja wa Port Gentil.

Alisema kuwa inasababisha majeraha kwa wachezaji.

"Hiyo ni funzo kwetu sisi kuhakikisha kuwa tunadhibiti hali ya baadaye ya mchezo huo'' Katibu mkuu wa Caf Hicham El Amrani, ameiambia BBC Michezo.

"Tunachukulia swala hilo kwa uzito mkubwa.

"Haja kuu ni kuhakikisha unafanya kazi moja kwa moja na kamati kuu andalizi ya michuano hiyo, hata kabla ya uwanja kuandaliwa na nyasi kuwekwa ili kutoa ujuzi wako, hasa kuwapa orodha ya watoa huduma''.

Haki miliki ya picha JUSTIN TALLIS
Image caption Mashabiki wa Cameroon mjini Yaounde, wakitazama timu yao katika mchuano wa fainali ya kombe la mataifa bingwa Afrika, dhidi ya Misri

Muda mfupi mno ulitolewa kwa Gabon kuwa mwenyeji wa fainali ya michuano hiyo mnamo April 2015, baada ya uwenyeji kuondolewa Libya, taifa ambalo lilikuwa liandae mashindano ya mwaka huu, baada ya kutokea mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

El Amrani, amesema kuwa mazungumzo tayari yameanza, kuandaa viwanja vya michezo vitakavyotumika kuandaa mchuano wa kombe la mataifa bingwa Afrika mwaka 2019 nchini Cameroon, taifa ambalo timu yake ilinyakuwa ubingwa wa kombe hilo mwaka huu.