Muhtasari: Habari kuu leo Ijumaa

Miongoni mwa habari nyingine kuu leo, mmoja wa waogeleaji wa Marekani amekiri walihadaa kuhusu kisa cha kuporwa Brazil na UN imekiri ilichangia mlipuko wa kipindupindu nchini Haiti.

1. Mmarekani akiri kuhadaa nchini Brazil

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Waogeleaji Jack Conger (kushoto) na Gunnar Bentz walizuiwa kuondoka Rio

Polisi wa Brazil wamesema kuwa mmoja kati ya waogeleaji wa Marekani walioshiriki katika Olimpiki amekiri, baada ya kuhojiwa, kuwa madai yao kwamba waliibiwa katika mji mkuu wa Rio ni uongo. Polisi wanasema kuwa wana ushahidi kwamba mmoja kati ya waogeleaji hao aliharibu choo kimoja katika kituo cha petroli jijini Rio.

2. UN ilichangia mlipuko wa kipindupindu Haiti

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Watu 10,000 walifariki wakati wa mkurupuko wa kipindupindu Haiti mwaka 2010

Kwa mara ya kwanza Umoja wa Mataifa umekiri kuwa ulichangia kwa kiasi kikubwa katika kulipuka kwa kipindupindu nchini Haiti miaka sita iliyopita ambapo zaidi ya watu 10,000 walifariki nchini humo.

Uchunguzi wa Kisayansi, mara kwa mara, umeonyesha kuwa wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kutoka Nepal walikuwa chanzo cha mlipuko huo ingawa Umoja wa Mataifa umekuwa wakati wote ukikanusha madai hayo.

3. Urusi kuunga mkono kusitishwa vita Aleppo

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Misaada ya kibinadamu inahitajika kwa dharura Aleppo, UN imesema

Urusi imesema kuwa iko tayari kuunga mkono usitishaji wa mapigano katika mji wa Aleppo kwa saa 24 kufuatia ombi lililotolewa na Balozi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria.

Balozi huyo, Staffan de Mistura, alifurahia uamuzi huo wa Urusi, lakini akaeleza kuwa kilichosalia ni wajibu wa Urusi kuwasilisha ahadi hiyo.

4. Tume ya haki yasema 22 waliuawa kinyama Mexico

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Polisi waliuawa jumla ya watu 42 katika kipindi cha saa tatu

Tume ya Haki za binadamu ya Mexico imesema kuwa inaamini kuwa watu 22 waliuawa na maafisa wa polisi, wakati wa makabiliano katika jimbo la Magharibi la Michoacan mwaka uliopita. Jumla ya washukiwa 42 wa genge la ulanguzi wa madawa ya kulevya waliuawa pamoja na afisa mmoja wa polisi.

5. Marekani yakiri Iran ililipwa kuachilia mahabusu

Haki miliki ya picha AP
Image caption Marekani ililipa $400m kusaidia kuachiliwa kwa mahabusu watano

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imekiri kuwa ilitumia malipo ya Dola Milioni 400 kwa Iran kama kishawishi cha kuhakikisha kuwa Wamarekani waliokuwa wanazuiliwa nchini humo wanaachiliwa.

Hata hivyo Wizara hiyo inasema kuwa kiwango hicho cha pesa kilikuwa malipo ya deni la zamani na wala sio kikombozi kama wanavyodai Wabunge wa chama cha Republican.