Wajerumani washauriwa waweke akiba ya chakula

Haki miliki ya picha GETTY IMAGES
Image caption Chupa za maji mjini Munich: Mashambulio ya ugaidi yamechochea hofu kuhusu usalama wa taifa

Kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa Vita Baridi serikali ya Ujerumani imewashauri raia wa nchi hiyo kuweka akiba ya chakula na maji kwa ajili ya matumizi ya dharura ya taifa.

Baadhi ya wabunge wa upinzani wamesema dhana hiyo mpya ya ulinzi wa raia inayotarajiwa kuwasilishwa mbele ya kikao cha mawaziri Jumatano, ni vitisho visivyo na msingi.

Raia wanashauriwa kuweka akiba ya kutosha ya chakula wanachoweza kutumia kwa muda wa siku kumi, kwasababu mkasa unaweza kusababisha huduma za kitaifa kushindwa kumudu huduma zinazohitajika.

Wameshauriwa kuweka akiba ya maji ya siku tano... kiasi cha lita mbili kwa kila mtu kwa siku.

Wavuti wa habari wa ujerumani ,Frankfurter Allgemeine (FAZ) umesema dhana hii mpya ilichapishwa katika kurasa 69 za waraka wa wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani.

Waraka huo umesema "shambulio kwenye ardhi ya Ujerumani , linalohitaji ulinzi wa pamoja wa taifa, si rahisi litokee ". Lakini, ulisema , tisho la taifa kwa siku zijazo haliwezi kufahamika , kwa hivyo hatua za ku walinda raia ni muhimu.

Kutokana na hatua hiyo, raia wa Ujerumani wamekua wakitoa hisia zao kupitia mitandao ya kijamii hususan twitter kupitia alama ya leri -hashtag "Hamsterkaeufe" ikimaanisha, ''ununuzi wa hofu''

Mkuu wa shughuli za chama cha mrengo wa kushoto Die Linke , Dietmar Bartsch, katika bunge la Ujerumani alikosoa hatua hiyo akisema, "unaweza kuwachanganya watu na kuwafanya wachukue hatua nyinginye kama vile, kubana mauzo ya bidhaa ".

Haki miliki ya picha TWITTER
Image caption "#ununuzi wa hofu: Hivi ndivyo hali itakavyokua saa 2 baada ya kufunguliwa kwa duka la chakula ," alisema raia mmoja katika twitter

Naibu kiongozi wa chama cha Green katika bunge la Ujerumani, Konstantin von Notz, amesema kuwa ni jambo muhimu kuwafahamisha raia kuhusu wajibu wao wa kujilinda, suala ambalo halijawahi kuzungumziwa tangu mwaka 1995.

Lakini ameonya dhidi ya kukanganywa kwa ulinzi huo wa masuala ya kijamii na kutokea kwa harakati za kijeshi na kigaidi akisema, "sioni shambulio lolote linaloweza kudhibitiwa na kuwepo kwa akiba ya chakula ya umma".