Watu 73 wafariki kutokana na tetemeko la ardhi Italia

Tetemeko la ardhi Italia Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Majumba mengi yameporoka katika miji iliyo eneo la Umbria

Watu takriban 73 wamefariki baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi lenye nguvu ya 6.2 katika vipimo vya Richter maeneo yenye milima katikati mwa Italia.

Watu wengine wengi wamefukiwa chini ya vifusi.

Wengi wamefafiki katika kijiji cha Pescara del Tronto ambacho kimeharibiwa vibaya na inahofiwa kwamba idadi ya waliofariki huenda ikaongezeka.

Tetemeko hilo lilitokea mwendo wa saa tisa na dakika thelathini na sita usiku saa za Italia (01:36 GMT), 76 km (maili 47) kusini mashariki mwa mji wa Perugia, katika kina cha 10km (maili sita) chini ya ardhi, taasisi ya Marekani inayohusika na mitetemeko ya ardhi USGS imesema.

Mitetemeko ilisikika katika miji ya mbali kama vile Roma, Venice, Bologna na Naples. Mjini Roma, baadhi ya majumba yalitikisika kwa sekunde 20, kwa mujibu wa gazeti la La Repubblica.

Haki miliki ya picha Reuters

Mji wa Amatrice nao pia uliharibiwa vibaya. Watu wanne wanahofiwa kufariki katika mji jirani wa Accumoli.

Eneo hilo, ambalo linapatikana katikati mwa mikoa ya Umbria, Lazio na Marche, ni maarufu sana kwa watalii na kuna wageni wengi waliokuwa eneo hilo kipindi hiki cha shughuli nyingi za kitalii.

Kitovu cha tetemeko hilo kilikuwa katika mji wa Norcia, karibu na Perugia.

Waziri mkuu wa Italia, Matteo Renzi, amesema serikali yake inaendelea kuwasiliana na taasisi za kiraia la ulinzi wa nchi hiyo.

Meya wa mji wa Amatrice Sergio Perozzi ameambia kituo cha redio cha serikali cha RAI kwamba mji huo umeharibiwa vibaya.

"Barabara za kuingia na kutoka mjini hazipitiki. Nusu ya mji imeharibiwa. Watu wamefukiwa chini ya vifusiā€¦ kumetokea maporomoko ya ardhi na kuna daraja moja ambalo huenda likaporomoka," amesema.

Shirika la kulinda raia Italia limeeleza tetemeko hilo kuwa "mbaya".

Haki miliki ya picha Reuters

Tetemeko hilo awali lilikisiwa kuwa la ukubwa wa 6.4. Lilifuatwa na mitetemeko mingine mikubwa, gazeti la

La Repubblica limeripoti.

USGS wamesema uharibifu huenda ukawa mkubwa.

Mwaka 2009, tetemeko la ardhi la nguvu ya 6.3 lilitokea eneo la Aquila, na kusikika pia katika mji wa Roma. Watu zaidi ya 300 walifariki.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii