Aliyempa mbwa wake jina 'Buhari' ashtakiwa Nigeria

Muhammadu Buhari Haki miliki ya picha AFP
Image caption Muhammadu Buhari

Mwanamume mmoja raia wa Nigeria ambaye alimpa mbwa wake jina la rais wa taifa hilo Muhammadu Buhari kwa kumuandika mbwa huyo jina 'Buhari' kwenye mwili wake amekamatwa kwa kosa la kutatiza amani.

Joe Fortemose Chinakwe, alimtembeza 'Buhari' katika sehemu ambazo Rais Buhari ni maarufu sana, polisi wanasema.

Maafisa wa polisi walisema walihofia hilo lingesababisha mvutano baina ya watu, ingawaje mwanamume huyo alisema ilikuwa kama njia ya kumsaidia Rais Buhari.

Chinakwe amepewa dhamana lakini amesalia kizimbani hadi atakapopata pesa za kulipa dhamana hiyo, ripoti zinasema.

Bw Chinakwe, mwenye umri wa miaka 30, amesema alimpa mbwa huyo Buhari kwa sababu alimpenda Rais Muhammadu Buhari kwa miaka mingi tangu akiwa mkuu wa jeshi wa taifa hilo.