Waliofariki Italia wafika 247, manusura watafutwa

Pescara del Tronto Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Nyumba nyingi Pescara del Tronto ziliporomoka

Idadi ya watu waliofariki kutokana na tetemeko la ardhi katikati mwa Italia mapema Jumatano imefika 247 huku manusura wakiendelea kutafutwa.

Maafisa wa uokoaji wanaendelea na juhudi za kutafuta manusura na miili kwenye vifusi.

Tetemeko hilo la nguvu ya 6.2 katika vipimo vya Richter liliharibu vibaya miji ya Amatrice, Accumoli na Pescara del Tronto ambapo watu wengi walifariki.

Maafisa wa uokoaji waliendelea na juhudi za kuwatafuta manusura usiku, lakini wakati mmoja walitatizwa na mitetemeko mingine iliyotokea na kutikisa majumba yaliyosalia yakiwa bado wima.

Eneo lililokumbwa na tetemeko hilo ni milimani katika majimbo ya Umbria, Lazio na Marche.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Manusura eneo la Amatrice wakesha chini ya mti usiku

Kitovu cha tetemeko hilo kilikuwa karibu na Norcia, kilomita 170 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Roma.

Mahema yamewekwa kuwasaidia watu walioachwa bila makao.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii