Bunge la Tunisia laidhinisha serikali ya Youssef Chahed

Waziri mkuu wa Tunisia Youssef Chahed Haki miliki ya picha AP
Image caption Waziri mkuu wa Tunisia Youssef Chahed

Bunge nchini Tunisia imepiga kura ya kuidhinisha serikali mpya, itakayoanza kutekeleza majukumu yake siku chache zijazo.

Serikali ya umoja inayoongozwa na waziri mkuu, Youssef Chahed, iliungwa mkono na wabunge 167, kati ya wabunge 217.

Serikali ya bwana Chahed inashirikisha wahafidhina wa kiislamu, wanasiasa wa mrengo wa kushoto, wanaharakati wa vyama vya wafanyikazi na wanasiasa binafsi.

Bwana Chahed ameahidi kuchukua hatua dhabiti za kuimarisha uchumi wa taifa hilo pamoja na uslama.

Youssef Chahed, 40, ataandikisha historia ya taifa hilo kwa kuwa waziri mkuu aliye na umri mdogo sana tangu taifa hilo lipate uhuru wake kutoka kwa Ufaransa, mwaka 1956.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wabunge wengi waliidhinisha serikali mpya

Youssef Chahed, aliyekuwa waziri wa maswala ya ndani ya Tunisia aliteuliwa kuwa waziri mkuu baada ya aliyemtangulia kuondolewa kwenye kura ya kutokuwa na imani naye mwezi uliopita.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption zaidi ya theluthi ya vijana wa Tunisia hawana ajira.

Ukosefu wa ajira umekithiri tangu kutokea kwa mapinduzi mwaka 2011, baada ya rais Zine al-Abidine Ben Ali kuondolewa mamlakani.

Zaidi ya theluthi ya vijana wa taifa hilo hawana ajira.

Taifa hilo la Afrika kaskazini linajitahidi kurejesha fahari yake kama kivutio cha watalii, baada ya wapiganaji wa kiislamu kutekeleza mashambulizi mawili yaliyolenga raia wa kigeni.

Migomo na maandamano pia yameathiri sekta muhimu ya madini ya phosphate.

Mapinduzi ya Tunisia yalikuwa ya kwanza katika msururu wa mapinduzi ya mataifa ya kiarabu, na huwa yanasifiwa kwa ufanisi wake, ambapo sasa taifa hilo linatumia mfumo wa kidemokrasia wa uongozi wa bunge.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii