Usafiri wa helikopta kuzinduliwa Nairobi kuepuka msongamano wa magari

Msongamano wa Magari jijini Nairobi
Image caption Kampuni ya huduma za teksi, Uber - kwa ushirikiana na makampuni ya helikopta binafsi wametangaza kuwa wataanza kuwasafirisha watu mara moja.

Wakenya wanaoishi jijini Nairobi hivi karibuni watakuwa na mbinu mpya ya kukwepa msongano wa magari, mara hii wakitumia usafiri wa helikopta.

Kampuni ya huduma za teksi, Uber - kwa ushirikiana na makampuni ya helikopta binafsi wametangaza kuwa wataanza kuwasafirisha watu mara moja.

Usafiri wa helikopta za Uber unatarajiwa kuwavutia wengi, licha ya kwamba kampuni ya Uber inakabiliwa na changamoto tangu ilipozinduliwa nchini Kenya mapema mwaka huu.

Uber ilikumbwa na mashambulizi yaliyoharibu magari yake ya teksi kutoka kwa mahasimu wao katika biashara ya teksi.

Ushirikiano baina ya makampuni mawili ya Uber na ile ya umiliki wa helikopta binafsi ni wa kwanza wa aina yake nchini Kenya kwa kuwawezesha watu binafsi kununua tiketi ya usafiri kwa njia ya internet.

Safari zinatarajiwa kuchukua mwendo wa dakika 20, ikilinganishwa na saa nyingi mtu anazokaa kwenye msururu wa magari.

Image caption Jiji la Nairobi limekuwa likikumbwa na msongamano mkubwa wa magari hususan pale unapotembelewa na viongozi wakuu wa nchi wakati wa mikutano ya kimataifa.

Washirika wa Uber kampuni ya Corporate Helicopters -tayari wamekuwa wakiendesha safari za nje ya jiji la Nairoi kutoka uwanja mdogo wa ndege wa Wilson kwa wasafiri wanaotaka kukwepa msongamano mkubwa wa magari jijini Nairobi.

Jiji la Nairobi limekuwa likikumbwa na msongamano mkubwa wa magari hususan pale unapotembelewa na viongozi wakuu wa nchi wakati wa mikutano ya kimataifa.

Kulikuwa na malalamiko ya umma mapema mwaka huu wakati wa ziara ya waziri mkuu wa Israeli Binyamin Netanyahu ambapo bara bara nyingi zilifungwa kwa ajili ya kuboresha usalama wake .

Raia wengi wa Kenya hawana uwezo wa kutumia usafiri wa helikopta , lakini kampuni ya Uber inasema teksi zake zitawasafirisha hadi kwenye maeneo ya muhimu.

Kwa sasa safari moja ya ndege jijini Nairobi inagharimu hadi dola 300, lakini haiko bado haijafahamika ni kiwango gani cha nauli kitakachotozwa na Uber licha ya kwamba inasema itakuwa nafuu.

Huduma hiyo ya usafiri wa helikopta itatolewa katika miji ya Nairobi na Mombasa.