Filamu 10 unazofaa kutazama Septemba

Idhaa ya BBC inayoangazia masuala ya sanaa na utamaduni, BBC Culture, imechagulia filamu 10 mashuhuri ambazo zitazinduliwa mwezi huu ambazo ni pamoja na moja ya vibonzo, nyingine kuhusu maisha ya watu na nyingine makala.

Ndizo hizi hapa:

Queen of Katwe

Haki miliki ya picha Walt Disney Studios Motion Pictures

Queen of Katwe inasimulia maisha halisi ya Phiona Mutesi, msichana aliyetoka kuuza mahindi barabara za Kampala na mwishowe akawa bingwa wa chess. Itazinduliwa katika Tamasha ya Kimataifa ya Filamu ya Toronto. Mwelekezi wake ni Mira Nair (Monsoon Wedding), na waigizaji nyota ni David Oyelowo na Lupita Nyong'o.

Itaanza kuoneshwa kwenye kumbi za sinema 23 Septemba Brazil na Marekani. (Hisani: Walt Disney Studios Motion Pictures)

Sausage Party

Haki miliki ya picha Columbia Pictures

Kidogo inaonekana kama filamu ya watoto lakini walioandaa Sausage Party wanaonya kuwa ni ya watu wazima pekee. Ni filamu ya ucheshi wa kiwango kingine. Seth Rogen, Kristen Wiig na James Franco wanaigiza kama soseji na bidhaa wenzake marafiki katika duka moja la jumla. Itazinduliwa 2 Septemba Uingereza na Ireland na 8 Septemba Uholanzi na Urusi (Hisani: Columbia Pictures)

The Light Between Oceans

Haki miliki ya picha Touchstone Pictures

Inawashirikisha nyota wa uigizaji Michael Fassbender na Alicia Vikander na inaangazia maisha ya kipanezi ya miaka 1920 ikifuata riwaya ya kwanza iliyoandikwa na ML Stedman. Itazinduliwa 2 Septemba nchini Canada na Marekani na 8 Septemba nchini Argentina, Serbia na Ujerumani. (Hisani: Touchstone Pictures)

The Lovers and The Despot

Haki miliki ya picha Magnolia Pictures

Hii ni makala inayoangazia maisha Korea Kaskazini. Ina mahojiano na nyota wa filamu wa zamani wa Korea Kusini Choi Eun-hee, ambaye pamoja na mumewe walitekwa na maajenti wa kiongozi wa zamani wa Korea Kaskazini Kim Jong-Il na kutakiwa kuandaa na kuvumisha filamu Korea Kaskazini.

Itaingia kwenye kumbi za sinema Uingereza na Marekani 23 Septemba na 24 Septemba Japan. (Hisani: Magnolia Pictures)

Things to Come

Haki miliki ya picha CG Cinema

Ni filamu inayoangazia maisha ya mwalimu wa falsafa wa umri wa makamo na inaonesha maisha yake yanavyobadilika baada yake kuachwa na mumewe. Mwelekezi wake ni Mia Hansen-Løve (Eden) na waigizaji nyota Isabelle Huppert na André Marcon.Itazinduliwa 2 Septemba Uingereza na Ireland na 23 Septemba nchini Uhispania. (Hisani: CG Cinema)

Bridget Jones's Baby

Haki miliki ya picha United Pictures International

Ni msururu wa filamu za maisha ya kifamilia za Bridget Jones's Diary na Bridget Jones: The Edge of Reason. Baada ya kubeba mimba miaka 12, yuko tayari kujifungua. Waigizaji nyota Renée Zellweger na Colin Firth wanaungana tena.

Itatolewa 15 Septemba nchini Singapore, Serbia na Ureno na 22 Septemba nchini Brazil, Italia na Thailand. (Hisani: United Pictures International)

Sully

Haki miliki ya picha Warner Bros

Ni simulizi ya kisa cha Captain Chesley 'Sully' Sullenberger ambaye akiwa kwenye usukani wa ndege ya US Airways safari nambari 1549, ndege hiyo inagonga bata bukini na kuharibika injini. Hakuna uwanja wa ndege ulio karibu anaoweza kutua. Mwelekezi wa filamu ni Clint Eastwood na Sully anaigizwa na Tom Hanks.

Itazinduliwa 8 Septemba nchini Denmark, Hungary na Israel na 9 Septemba nchini Finland na Marekani. (Hisani: Warner Bros)

Miss Peregrine's Home for Peculiar Children

Haki miliki ya picha 20th Century Fox

Imetokana na riwaya mashuhuri ya 2011 YA yake Ransom Riggs ambayo inaangazia mvulana anayegundua kituo cha mayatima ambacho mayatima walio huko wana nguvu za mazingaombwe.

Wahusika ni Jane Goldman (Kick Ass), Tim Burton na Eva Green.

Itaingia kwenye kumbi za sinema 29 Septemba Denmark, Hong Kong na Cambodia na 30 Septemba Uhispania, Marekani na Sweden. (Hisani: 20th Century Fox)

Blair Witch

Haki miliki ya picha Lionsgate

Miaka 17 baada ya filamu ya kwanza ya kuogofya kuzinduliwa, filamu za Blair Which zinarejea.

Itazinduliwa 16 Septemba nchini Canada, Norway na Marekani. (Hisani: Lionsgate).

The Beatles: Eight Days a Week - The Touring Years

Haki miliki ya picha Alamy

Baada ya utumbuizaji waouliowajengea jina katika kipindi cha Ed Sullivan Show mwaka 1964, The Beatles walitembea pande mbalimbali duniani wakitumbuiza. FIlamu hii ni simulizi ya yaliyojiri katika nchi 15 na majiji 90 waliyotembelea. Mwelekezi ni Ron Howard (Rush, A Beautiful Mind). Imeidhinishwa na Paul McCartney, Ringo Starr, Yoko Ono Lennon na Olivia Harrison. Itaanza kuoneshwa 15 Septemba nchini Ujerumani, Ufaransa na Australia na 22 Septemba nchini Japan. (Alamy)