Wabunge wataka matumizi ya bangi yahalalishwe Uingereza

Bangi Haki miliki ya picha Thinkstock

Kundi moja la wabunge nchini Uingereza limetoa wito wa kuhalalishwa kwa matumizi ya bangi kwa sababu za kimatibabu nchini humo.

Kundi hilo linalojumuisha wabunge kutoka vyama mbalimbali vya kisiasa, na ambalo limekuwa likitetea mageuzi kuhusu matumizi ya dawa, limesema kuna ushahidi bayana kwamba matumizi ya bangi huwa na manufaa katika kutibu baadhi ya matatizo ya kiafya, yakiwemo maumivu makali na kutatizwa na wasiwasi.

Wabunge hao wanasema tayari maelfu ya watu huvunja sheria kwa sasa na kutumia bangi kama dawa.

Lakini wizara ya mambo ya ndani nchini humo imesema kufikia sasa hakuna mipango ya kuhalalisha matumizi ya "dawa hiyo hatari".

Mmea wa bangi huwa na karibu kemikali 60.

Wabunge hao wanataka serikali iondoe bangi kutoka kwa kitengo nambari moja hadi kitengo nambari nne.

Kitengo hicho kina dawa nyingine zikiwemo homoni, vitamini na dawa za kupunguza maumivu.

Hii itawawezesha madaktari kumpendekezea mgonjwa kutumia bangi kama dawa.

Haki miliki ya picha SPL

Taasisi ya Taifa ya Afya Uingereza imetahadharisha kwamba bangi huwa na madhara makubwa kwa mwili, ikiwemo kutatiza uwezo wa mtu kuendesha gari na kudhuru mapafu na afya ya kiakili, kuathiri uwezo wa mtu kuzaa na kuathiri pia watoto ambao hawajazaliwa.

Bangi pia huwa na kiwango cha utegemezi cha 9%, ingawa si cha juu sana ukilinganisha na tumbaku 32% na pombe 15%.

Lakini wabunge hao wanasema wametathmini ushahidi kutoka kwa wagonjwa 623 pamoja na kuzungumza na wataalamu kutoka nchi nyingi duniani na wamegundua bangi inaweza kufaa sana kama dawa.

Matumizi ya bangi kwa sababu za kimatibabu yamehalalishwa katika majimbo 24 nchini Marekani na pia nchini Canada na Israel.

Kadhalika, nchi 11 kwa sasa huruhusu kutumiwa kwa bangi kwa sababu za kiafya.