Pande pinzani zakubaliana kuhusu mpango wa uchaguzi DRC

Rais wa DRC Joseph Kabila Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais wa DRC Joseph Kabila

Wapatanishi katika mazungumzo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanasema kuwa pande husika zimekubali kuhusu mpangilio wa uchaguzi utakavyofanyika,swala ambalo lilifanya upinzani kujiondoa katika meza ya mazungumzo mapema wiki hii.

Tuhuma kwamba huenda rais Joseph kabila akajaribu kujiongezea muda wa kutawala baada ya muhula wake wa pili kukamilika imesababisha mgogoro wa kisiasa nchini humo.

Waziri wa haki Alexis Thambwe Mwamba amesema kuwa chini ya makubaliano hayo ambayo hayajatiwa saini,uchaguzi wa urais,ule wa kitaifa pamoja na ule wa kijimbo itafanyika siku moja.

Bwana Mwamba ameongezea kwa serikali ya mda ikishirikisha wanachama wa upinzani itabuniwa ili kusaidia kutatua mgogoro huo wa uchaguzi.

Makundi mengi ya upinzani yamesusia mazungumzo hayo ili kutohalalisha mchakato wa mazungumzo hayo.

Mapema shirika la Amnesty International lilichapisha ripoti ambayo ilishtumu mamlaka ya DRC kwa kupanga njama za kuwakandamiza wapinzani wa Kabila.