Korea Kaskazini yaujaribu mtambo wa roketi

Kim Jong-un Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kim Jong-un alisimamia kutekelezwa kwa jaribio hilo

Korea Kaskazini "imefanikiwa" kuufanyia majaribio mtambo mpya wa kurusha roketi ambao unaweza kutumiwa kurusha setilaiti angani, shirka la habari la serikali nchini humo limesema.

Kiongozi wa taifa hili Kim Jong-un, amewataka wanasayansi na wahandisi nchini humo kufanya maandalizi ya kurusha setilaiti angani haraka iwezekanavyo.

Bw Kim mwenyewe alisimamia kufanywa kwa jaribio hilo eneo la Sohae, shirika la KCNA limesema.

Jaribio hilo lililotekelezwa ardhini ndilo la karibuni zaidi katika msururu wa majaribio yanayoonekana kuwa na lengo la kuimarisha uwezo wa taifa hilo kurusha makombora ambayo yametekelezwa na Pyongyang mwaka huu.

Korea Kaskazini imesisitiza kwamba mpango wake wa kutaka kutuma mitambo anga za juu una malengo ya kisayansi pekee lakini Marekani, Korea Kusini na China (mshirika wa Pyongyang) wote wanaamini kwamba mpango huo wa kurusha roketi una lengo la kuiwezesha Korea Kaskazini kurusha makombora ya masafa marefu.

Hayo yakijiri, Marekani na Uchina wameafikiana kushirikiana zaidi katika Umoja wa Mataifa kuangazia jaribio la tano la nyuklia lililotekelezwa na Korea Kaskazini hivi majuzi. Maafisa wa nchi hizo mbili wameanza mashauriano kuhusu uwezekano wa kuiwekea Korea Kaskazini vikwazo zaidi.

Jaribio hilo linaaminika kuwa la bomu kubwa zaidi kuwahi kutekelezwa na Korea Kaskazini kufikia sasa.

Korea Kaskazini mara kwa mara hutoa madai kuhusu ufanisi wake katika kuunda silaha za nyuklia na makombora, lakini wachanguzi wengi wanasema ni vigumu kubaini ukweli wa mengi ya madai hayo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waziri Mkuu wa China Li Keqiang alikutana na Rais wa Marekani Barack Obama pambizoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa New York

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii