Yahoo walichunguza barua pepe kwa niaba ya Marekani

Yahoo Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Majuzi ilibainika kwamba wadukuzi waliiba maelezo ya watumiaji 500 millioni wa Yahoo

Yahoo walichunguza mamilioni ya barua pepe za watu kwa niaba ya serikali ya Marekani, ripoti ya shirika la habari la Reuters inasema.

Shirika hilo la habari linasema kampuni hiyo iliunda programu maalum mwaka jana na kuitumia ili kutimiza ombi rasmi kutoka kwa serikali ya Marekani.

"Yahoo ni kampuni inayofuata sheria, na hutii sheria za Marekani," kampuni hiyo imesema kupitia taarifa kwa BBC.

Reuters wanasema maombi yalitoka kwa Shirika la Usalama wa Taifa (NSA) au kwa FBI.

Programu iliyoundwa na Yahoo ilikuwa inachunguza uwepo wa tarakimu, alfabeti au ishara fulani za maandishi kwenye barua pepe zilizokuwa zikipokelewa.

Hata hivyo, Reuters wanasema hawakuweza kubaini ni habari za aina gani zilizokabidhiwa kwa maafisa wa Marekani au iwapo kampuni nyingine zinazotoa huduma mtandaoni zilihusika.

Tuhuma hizo zinatokea chini ya wiki mbili baada ya kubainika kwamba wadukuzi waliiba maelezo ya watumiaji 500 milioni wa mtandao huo.

Yahoo kwa sasa imo kwenye mchakato wa kununuliwa na kampuni ya Verizon Communications kwa jumla ya $4.8bn (£3.8bn).

Kampuni hiyo ya Verizon hata hivyo imekataa kuzungumzia tuhuma hizi mpya.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii