Antonio Guterres, atakayeongoza UN, ni nani?

Antonio Guterres amechaguliwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Haki miliki ya picha AFP
Image caption Umoja wa Mataifa umechagua Katibu Mkuu mpya- Antonio Guterres

Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa amechaguliwa. Antonio Guterres ndiye atakayemrithi Katibu Mkuu wa sasa anayeondoka Ban Ki Moon.

Kumekuwa na wito kwa Umoja huo kutoa nafasi kwa mwanamke kuongoza wakati huu, hata hivyo wanamama hawakubahatika.

Guterres anatarajiwa kuchukua hatamu za kuongoza Umoja wa Mataifa mwezi Januari mwakani.

Guterres alizaliwa mjini Lisbon Ureno mwaka wa 1949. Alisomea shahada ya uhandisi na Fisikia katika Taasisi ya 'Superior T├ęcnico'.

Baada ya kufuzu hapo mwaka wa 1971 alianza kuwa mkufunzi kwa miaka michache ambapo alihudumu katika taasisi za kikatoliki.

Mnamo mwaka wa 1974 alijiunga na chama cha Kisocialisiti na kuwa mwanasiasa wakati ambapo Ureno ulimaliza utawala wa kiimla uliodumu kwa miongo mitano.

Alichaguliwa Katibu Mkuu wa chama hicho mwaka wa 1995 na kuhudumu wadhifa huo hadi mwaka wa 2002.

Antonio Guterres anazungumza kwa ufasaha lugha za Kiingereza, Kihispania na Kifaransa.

Haki miliki ya picha UN/AP
Image caption Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ndilo huchagua Katibu Mkuu

Alijiunga na ulingo wa diplomasia ya dunia mwaka wa 2005 alipochaguliwa Kamishina wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi-UNHCR.

Chini ya uongozi wake katika UNHCR, alipunguza idadi ya wafanyikazi waliokuwa katika makao makuu mjini Geneva, na badala yake akaweka juhudi za kuhamasisha wafanyikazi wa UNHCR kukaa karibu na wakimbizi pamoja na kufahamu jinsi ya kukabiliana na majangwa.

Alisifika sana kwa juhudi zake kushawishi dola tajiri duniani kusaidia wakimbizi wa vita na waathiriwa wa majanga.

Antonio Guterres, ana miaka 67 na baba ya watoto wawili kutoka ndoa yake ya kwanza. Mkewe wa kwanza alifariki dunia mwaka wa 1998.

Alioa tena mwaka wa 2001.