23 wauawa baada ya kambi ya wakimbizi kushambuliwa CAR

Mamilioni ya watu wameachwa bila ya makaazi CAR Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mamilioni ya watu wameachwa bila ya makaazi CAR

Takriban watu 23 wameuawa katika Jamhuri ya Afrika ya kati katika shambulio dhidi ya kambi ya wakimbizi ya Umoja wa mataifa nchini humo, shirika la habari la Reuters linaarifu.

Shambulio hilo limetekelezwa usiku Jumatano na wafuasi wa kundi la waasi wa kiislamu Seleka, kwa mujibu wa maafisa wa Umoja wa mataifa walio nukuliwa na Reuters.

Wanamgambo hao wanatuhumiwa kuwaua wakimbizi 13 kabla ya 10 baadhi yao kupigwa risasi na wanajeshi wa Umoja wa mataifa nchini humo, Munisca, walio ingilia kati.

Mamia ya wakaazi wa vijiji walio ingiwa uoga ambao tayari wameachwa bila makaazi kutokana na ghasia za awali, wamekimbilia kuelekea kwenye kambi hiyo ya Umoja wa mataifa.

Ghasia hizi ni za karibuni katika Jamhuri ya Afrika ya kati ambayo imekumbwa na vita tangu mapema 2013 wakati waasi wa Seleka walipompindua rais aliyekuwepo, Francois Bozize.

Jamhuri ya Afrika ya kati imeathirika na ghasia za kikabila tangu waasi wa Seleka kuchukua uongozi mnamo Mach 2013.

Kundi jingine lenye wanamgambo wa kikristo linalojiita anti-Balaka, liliingia vitani dhidi ya kundi la Seleka.