Sheria mpya Indonesia 'itamaliza visa vya unajisi'

Rais Joko Widodo Haki miliki ya picha AFP/GETTY

Huenda Indonesia ikamaliza visa vya unajisi kwa sheria yake mpya ya kutumia kemikali kuwahasi wahalifu wanaowanyanyasa watoto kingono, rais Joko Widodo ameiambia BBC.

Amesema Indonesia inaheshimu haki za binaadamu lakini hakuna msamaha ikifika katika suala la kuwaadhibu wahalifu wa uovu huo wa kingono.

Indonesia imepitisha sheria zilizoibua utata mzozo mapema mwezi huu, na kuidhinisha kutumiwa kemikali kuhasi wanaume na hivyo kusitisha hamu ya ngono kwa wanaotekeleza unajisi.

Sheria hizo zimezusha mjadala mkali bungeni.

Muungano wa madaktari nchini humo unasema madaktari wasihusike, kwani mpango huo unakwenda kinyume na maadili ya kitabibu.

Mpango huo unahusisha kutumia kemikali kuwahasi wahusika, pasi na kukatwa sehemu za siri.

Rais Widodo amesema "katiba yetu inaheshimu haki za binadamu, lakini likija suala la uhalifu wa kingono hakuna namna".

"Tuna nguvu na tutalishikilia hilo. Tutatoa adhabu kali kwa uhalifu wa kingono."

Ameongeza: "Kwa maoni yangu ... mpango huu wa kemikali iwapo tutaushinikiza, utasaidia kupunguza uhalifu wa kingono na kumliza anayetekeleza unajisi hatimaye."

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kumeshuhudiwa visa vingi vya ulawiti wa watoto Indonesia

'Mpango wa kutumia kemikali hautofaulu na ni kinyume cha hali za binaadamu' - Muungano wa madaktari Indonesia

Huwezi kusitisha tatizo la unajisi wa watoto kwa kutumia kemikali.

Mpango huo utadumu kwa muda gani? Tuseme mgonjwa atatumia mbinu hiyo kwa miaka mitatu akiwa gerezani, lakini akitoka anaweza kwenda kwa dadaktari akafanyiwa marekebisho kwa kutumia dawa za homoni.

Zaidi ya hayo, adhabu hiyo haiwezi kufanywa ila na dakatri, kwa sababu ni lazima tufuate maadili ya utabibu. Unapokuwa daktari, unakula kiapo kutowadhuru binadamu.

Ujumbe wangu kwa madakatri wote Indonesia ni kuwa ili mradi wewe ni daktari huwezi kufanya hivyo hata kama serikali inasema ni kwa sababu ni kuwaadhibu walawiti.

Ina madhara na ni kinyume na haki za binaadamu.

Dr Prijo Sidipratomo ni mwenyekiti wa kamati ya maadili ya utabibu katika muungano wa madaktari Indonesia.