Trump asema hatakubali matokeo ya uchaguzi akishindwa

Trump na Clinton Haki miliki ya picha Getty Images

Mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha Republican Donald Trump amesema kuwa atakubali matokeo ya uchaguzi wa urais nchini Marekani ''iwapo atashinda''.

Amesema kuwa atakubali tu matokeo ya moja kwa moja yasiyo na udanganyifu wowote akiongezea kuwa ana haki ya kupinga matokeo hayo iwapo yatakuwa na utata.

Alionekana katika mkutano mjini Delaware jimbo la Ohio, akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya mjadala wa tatu wa urais dhidi ya mpinzani wake wa chama cha Democratic Hillary Clinton.

Bw Trump amekuwa akikosolewa kwa kusema kuwa hatakubali matokeo ya uchaguzi huo.

Donald Trump alikataa kuahidi kukubali matokeo ya uchaguzi iwapo atashindwa, katika mjadala wa mwisho wa urais dhidi ya Hillary Clinton Las Vegas.

"Nitakuambia wakati huo," alimwambia muendesha mjadala Chris Wallace.

Kwa siku kadhaa amedai kuwa kuna 'udanganyifu' katika uchaguzi huo.

Mjadala huo wa televisheni Las Vegas uliendeleza uhasama katika kampeni huku Trump akimuita Bi Clinton "mwanamke muovu".

Kura za kutafuta maoni zinaonyesha Trump amepoteza umaarufu katika majimbo makuu baada ya kukabiliwa na tuhuma za unyanyasaji wa kingono.

Mjadala huo wa mwisho wa umefanyika wiki tatu kabla ya siku ya uchaguzi Novemba 8.

Wagombea hao walikataa kusalimiana kwa mikono kabla na baada ya majibizano hayo ya kisiasa, hatua iliyofungua kile ambacho baadaye kiligeuka kuwa mjadala wa kelele na kukatizana kauli.

Trump alitoa ahadi kwa wanachama wa Republican kuwateua majaji wa mahakama ya juu zaidi wanaoegemea 'mrengo wa kihafidhina' watakaogeuza sheria kuu inayohalalisha uavyaji mimba Marekani na kulinda haki za kumiliki bunduki.

Haki miliki ya picha AP

Alisisitiza ahadi yake ya kuwarudisha nyumbani wahamiaji ambao hawakusajiliwa na kudhibiti mipaka ya Marekani.

Wakati huo huo, Bi Clinton ametangaza wazi kuwa atawatetea wapenzi wa jinsia moja, atalinda haki za kuavya mimba, atalenga kuinusha watu wa kipato cha wastani na kushinikiza kulipwa sawa kwa wanawake.

"Serikali haina shughuli yoyote katika maamuzi wanayofanya wanawake," alisema.

Katika mojawapo ya nyakati zilizokuwa na mvuto, Trump alikataa mara mbili kusema iwapo atakubali matokeo ya uchaguzi, hatua iliyobadili utamaduni wa muda mrefu wa wagombea wanaoshindwa kukubali matokeo baadaya kura kuhesabiwa.

"Hilo ni jambo la kuogofya," Clinton akajibu kwa ukali.

"Anaponda na kudharau demokrasia yetu. Na mimi kivyangu, nimeshangazwa kuwa mtu ambaye ni mgombea mteule wa mojawapo wa vyama viwili vikuu anaweza kuchukua msimamo wa aina hiyo."

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Trump alisindikizwa na familia yake baada ya mjadala kumalizika

Majibu ya Trump yamezua shutuma kali kutoka kwa seneta wa Republican Lindsey Graham, aliyesema mgombea huyo "hawajibiki ipasavyo kwa chama chake na taifa kwa kuendelea kuashiria kuwa anafanyiwa udanganyifu katika uchaguzi ujao," kwa mujibu wa taarifa.

Kauli nyingine kuu katika mjadala katika chuo kikuu cha Nevada ni :

  • Bi Clinton anasema Putin anataka Trump achaguliwe kwa sababu anataka kikaragosi awe rais wa Marekani.
  • "Tuna watu wabaya na tutawatoa," amesema Trump, aliposhinikiza ahadi yake ya kujenga ukuta mpakani.
  • Bi Clinton amesema ataidhinisha mpango mkubwa wa ajira kuwahi kushuhudiwa tangu vita vya pili vya dunia.
  • Trump ameashiria Bi Clinton na rais Barack Obama walipanga ghasia katika mkutano wake wa kisiasa Chicago mapema mwaka huu.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii