Nakumatt kuuza sehemu ya biashara yake

Nakumatt inasema inakumbwa na matatizo ya kiuchumi
Image caption Nakumatt inasema inakumbwa na matatizo ya kiuchumi

Moja ya kampuni inayomiliki maduka mengi ya jumla eneo la Afrika Mashariki ya Nakumatt inasema kuwa inauza sehemu ya biashara yake kutokana na changamoto za kiuchumi zinazoikumba.

Hii ni baada ya picha kusambaa kwenye mitandao zikionyesha rafu zisozokuwa na bidhaa katika duka la Nakumatt mjini Kampala Uganda.

Sasa mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Neel Shah, ameambia gazeti la Kenya Business Daily, kwamba mazungumzo yanaendelea ya kuuza asilimia 25 ya kampuni hiyo inayomilikiwa na familia.

Anasema kuwa hatua hiyo itasaidia kampuni hiyo kulipa madeni.

Hii ni kinyume na matarajio ya kampuni hiyo, ya kuzoa faida kubwa barani Afrika, wakati idadi ya watu wenye kipato cha katikati inazidi kuongezeka.

Nakumatt imelaumu hali mbaya ya kiuchumi na gharama ya juu ya uendeshaji kwa matatizo yanayoikumba sasa.

Sekta ya mauzo Afrika mashariki imedhihirisha kuwa ya kutamanika na pia yenye changamoto nyingi.

Lakini kampuni nyingi za kimataifa zimenawiri afrika mashariki.

Tayari kampuni ya Ufaransa Carrefour na Walmart ya Marekani zimefungua maduka yake jijini Nairobi Kenya.