Matokeo ya uchaguzi yatajulikana saa ngapi Marekani?

Wapiga kura eneo la Elyria, Ohio, 8 Novemba. Haki miliki ya picha Reuters

Maeneo mengi Marekani yalisubiri vituo vifungwe- sana kati ya 19:00 EST (24:00 GMT - Saa tisa usiku Afrika Mashariki) na 20:00 EST (01:00 GMT - Saa kumi usiku Afrika Mashariki) - kuanza kupokea matokeo na makadirio ya matokeo katika majimbo mbalimbali.

Vituo vya kura vilifungwa katika jimbo lenye umuhimu mkubwa uchaguzini kutokana na wingi wa wajumbe, California (55), ambayo ni ngome ya Democratic, pamoja na Oregon (7), Washington (12), Idaho (4) na Hawaii (4) mwendo wa saa 23:00 EST (04:00 GMT - Saa moja asubuhi Afrika Mashariki).

Kwa kutegemea hali, mshindi angetangazwa wakati huo, saa moja asubuhi Afrika Mashariki.

Lakini kutokana na ushindani mkali, bado matokeo yanasubiriwa.

Kwa kufuata desturi, aliyeshindwa anatarajiwa kutoa hotuba ya kukubali kushindwa muda mfupi baada ya mshindi kujulikana.

Ilikuwa saa 00:00 EST (05:00 GMT) mwaka 2012 na 2008. Hata hivyo, mwaka 2004, John Kerry alisubiri hadi siku iliyofuata kukubali kushindwa.

Ukuzingatia madai ya Bw Trump kwamba kura zitaibwa, iwapo atashindwa, huenda akataka kura zihesabiwe tena au akatae kukubali kushindwa. Hilo likifanyika, hakuna ajuaye mshindi wa urais atatangazwa wakati gani.

Rais mteule atasubiri hadi 20 Januari mwakani kuapishwa kuwa rais wa 45 wa Marekani. Hili limeelezwa vyema kwenye katiba. Rais mteule ataweka mkono wake kwenye Biblia na kula kiapo saa sita mchana. Kuanzia hapo, atachukua udhibiti wa serikali.

Wataingia pia White House. Kawaida, rais anayeondoka na mkewe huandalia Rais anayeingia mamlakani na mkewe dhifa kabla ya sherehe ya kuapishwa. Saa sita baadaye, familia mpya huingia ikulu.

Soma zaidi hapa: Mwongozo wa matukio makuu uchaguzi Marekani

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii