Wazimbabwe wa ughaibuni kutopiga kura

Raia wa Zimbabwe wanaoishi ughaibuni hawataruhusiwa kupiga kura katika mataifa wanayoishi katika uchaguzi ujao wa 2018 kulingana na tume ya uchaguzi nchini humo.
Hii ni licha ya marekebisho ya kikatiba ya mwaka 2013 ambayo yanatoa fursa kwa raia wa taifa hilo wanaoishi ng'ambo kushiriki katika uchaguzi.
Hii ni kwa sababu sheria mpya hazijaidhinishwa tangu katiba ifanyiwe marekebisho.
Hatua hiyo ya tume ni pigo kubwa kwa mamilioni wa raia wa taifa hilo wanaoishi ughaibuni ambapo wamepigana vita vya kutaka kushiriki wakiwa katika mataifa wanayoishi.
Upinzani umeshtumu hatua hiyo kama mpango wa serikali wa kuwanyima haki yao mamilioni wa raia wa Zimbabwe.
Rais Robert Mugabe ambaye amekuwa mamlakani tangu mwaka 1980 amesema kuwa atawania urais kwa muhula mwengine.
Raia milioni 4 wa Zimbabwe wameondoka nchini humo kutokana na mgogoro wa kisiasa pamoja na kiuchumi ambao umekumba taifa hilo kwa zaidi ya muongo mmoja.
Baadhi yao wamepatiwa hifadhi katika mataifa tofauti huku wengine wakiishi kinyume na sheria.