Raia wa Malawi na DRC miongoni mwa wanawake 100 wa BBC

Wanawake 100 wa BBC

Msimu wa Wanawake 100 wa BBC mwaka huu utakuletea makala za kusisimua kuhusu wanawake waliochukua msimamo wa ujasiri, mtazamo mpya kuhusu mambo yanayochukuliwa kuwa ya kawaida, ajuza wanaoongoza katika ushabiki na pia kukuingiza katika ulimwengu wa michezo ya kompyuta.

Makala nyingine zitaangazia wanaharakati weusi wanaotetea haki za wanawake au kukushirikisha katika tamasha ya moja kwa moja ya Wanawake 100 wa BBC.

Utasikia kutka kwa wanawake mashuhuri zaidi duniani lakini pia usikie kuhusu wanawake ambao hujawahi kuwasikia, ambao wana simulizi za kushangaza.

Miongoni wa Wanawake 100 walioshirikishwa mwaka huu kuna:

Aline Mukovi Neema, DR Congo

Kazi: Mwanafunzi/Mwanaharakati

Umri: 27

Ni mwanachama wa kundi la vijana mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao wanapigania mageuzi ya kisiasa.

"Licha ya hatari ambazo nakumbana nazo katika mfumo wa kisiasa, najaribu kupigania mageuzi," anasema.

Doaa el-Adl, Misri

Haki miliki ya picha Bassam Alzoghby

Kazi: Mchoraji vibonzo

Umri: 37

Ni mmoja wa wanawake wa kwanza katika tasnia hii inayotawaliwa na wanaume, na anaamini kwamba Sanaa ndiyo njia bora zaidi ya kuvunja kaida zinazokandamiza wanawake.

"Wanawake wa Kiarabu hukabiliwa na kizungumkuti cha kuamua kuwa mateka wa vita na mizozo, au kupinga hayo," anasema.

Dwi Handa, Indonesia

Kazi: Nyota wa Instagram

Miaka: 23

Ni mwanachama wa kundi jipya la watu wanaojiita 'Hipster Hijabis', ambao kupitia akaunti zao za Instagram, na wamekuwa na usemi katika mitindo miongoni mwa Waislamu. Wamekuwa wakialikwa maonesho ya mitindo na kulipwa kuvalia mitindo mipya.

"Tunahitaji kuwa na uwezo wa kujieleza na kujiangalia kwenye kioo na kuona kitu cha kuvutia na chenye uhai," anasema.

Egge Kande, Senegal

Kazi: Kiongozi katika jamii

Umri: 55

Ni mama wa watoto sita na ana wajukuu wanane. Yeye hushirikiana kwa karibu na walimu kuwashauri wasichana kuhusu masuala ya elimu kwa wasichana, ndoa za mapema na mimba za mapema.

"Sasa ninaweza kusimama kwenye paa na kusema yaliyo moyoni, bila woga na bila kulia," anasema.

Ellinah Ntombi Wamukoya, Swaziland

Kazi: Askofu

Umri: 65

Ndiye mwanamke wa kwanza kuteuliwa askofu katika Kanisa la Kiangilikana la Kusini mwa Afrika kusimamia jimbo la kanisa hilo la Swaziland.

"Nitawakilisha sifa za Mungu kama mama," anasema.

Funke-Bucknor Obruthe, Nigeria

Haki miliki ya picha Uwa Nnachi - BBC

Kazi: Kupanga harusi

Umri: 40

Hupanga kwa kina harusi za kufana za kifahari na za watu mashuhuri Nigeria, zinazohudhuria na wageni kati ya 500 na 2000.

"Kinachonichochea ni haja ya kuona watu wote wanaonizunguka wakifanikiwa, kuinua binadamu aliye karibu, na kutokubali kushindwa," anasema.

Gcina Mhlope, Afrika Kusini

Kazi: Mwandishi, Mshairi na Mtunzi wa michezo ya kuigiza

Umri: 58

Alihamasishwa na hadithi za nyanyake alipokuwa mdogo na sasa kazi zake za Sanaa zimeenea kote duniani.

"Nilishukuru sana kuoga katika mto usiokauka wa hadithi za kale," anasema.

Lucy Finch, Malawi

Kazi: Mwuguzi wa kutunza wagonjwa

Umri: 73

Mwanzilishi wa kituo pekee cha kutunza wagonjwa wenye maradhi yasiyopona nchini Malawi.

"Kuwatunza wagonjwa si tu kuhusu kuongeza maisha ya watu, bali kuongeza uhai katika siku ambazo wagonjwa wamesalia nazo," anasema.

Omotade Alalade, Nigeria

Kazi: Mwanzilishi wa wakfu wa wanawake tasa

Umri: 30

Mwanzilishi wa wakfu wa BeiBei Haven, ambao husaidia wanawake wanaotatizwa na utasa, wakfu ambao unaendelea kukua.

"Kusaidiziwa na kuongezewa maarifa husaidia sana wanawake kukabiliana na utasa na kupoteza watoto," anasema.

Saalumarada Thimmakka, India

Kazi: Mwanamazingira

Umri: 105

Amepanda zaidi ya miti 8,000 katika miaka 80, mradi aliouanzisha kwanza kama jibu kwa waliokuwa wanamkejeli kwa kutojaliwa watoto.

"Kila mtu, kuanzia watoto hadi wazee, anafaa kupanda na kutunza miti - hilo litatufaa sote," anasema.

Simone Biles, Marekani

Kazi: Mwanamichezo wa sarakasi

Umri: 19

Alishangaza wengi Michezo ya Olimpiki Rio, ambapo alishinda nishani nne za dhahabu. Alielezwa kuwa 'mwanasarakasi bora zaidi kuwahi kushuhudiwa'.

"Unaweza kujijengea bahati, kwa kufanya mazoezi," anasema.

Zoleka Mandela, Afrika Kusini

Kazi: Mwandishi/Mwanakampeni

Umri: 36

Ni mjukuu wa Nelson na Winnie Mandela, ambaye maisha yake yalikuwa magumu sana. Amewapoteza watoto wawili, akanusurika unyanyasaji wa kingono, akakabiliana na uraibu na kwa sasa anapokea matibabu ya saratani ya matiti.

Zulaikha Patel, Afrika Kusini

Kazi: Mwanafunzi

Umri: 13

Mwanafunzi wa Afrika Kusini ambaye aligeuka nembo ya vita dhidi ya sera ya shule moja ya upili iliyowalazimisha wasichana Waafrika kunyoosha nywele zao.

"Kunitaka nibadilishe nywele zangu ni kama kunitaka nifute weusi wangu," anasema.

Thuli Madonsela, Afrika Kusini

Haki miliki ya picha RAJESH JANTILAL

Kazi: Wakili

Umri: 54

Mlinzi wa Maslahi ya Umma Afrika Kusini 2009-2016, anayesifiwa sana kwa kukabiliana na utawala mbaya na ufisadi serikalini. Alikabiliana na maafisa waliotumia vibaya mamlaka serikalini na usimamizi wa mali ya umma.

„Iwapo kuna ukiukaji wa haki pahala fulani, hakuwezi kukawa na amani ya kudumu popote duniani," anasema.

Mada zinazohusiana