Masaibu ya wasichana katika mtaa wa mabanda jijini Nairobi

Felicia
Image caption Felicia akiendelea na kazi ya uoshaji magari

Felicia Onimbo ni mkaazi wa mtaa wa mabanda wa Majengo, jijini Nairobi mwenye umri wa miaka 23. Maisha katika mtaa huo ni ya shida hasa kwa wasichana.

Wasichana wengi katika mtaa huo hujiunga na biashara ya kuchuuza miili yao kwa wanaume, unywaji wa pombe na matumizi ya mihadarati, na wengi wao huwa hawamalizi shule.

Bi Felicia alipata mwanawe wa kwanza, baada ya kufanya biashara ya uuzaji wa mwili na hakuweza kukimu maisha yake, mwanawe, na hata familia yake kutokana na fedha duni alizokuwa akipata kutoka kwa kazi ya ufuaji nguo .

''Mimi na familia yangu tulikuwa tumezoea kula chakula cha jioni pekee. Na wakati mwingine tulikuwa tukipata kiamsha kinywa, ambayo ilikuwa ni chai ya mkandaa''

Felicia alikuwa akilipwa shilingi mia tano za Kenya (dola 5 za Kimarekani) na hata wakati mwengine alikuwa halipwi pesa zozote na wateja wake.

''Nilifanya mapenzi na watu wenye umri zaidi ya babangu ilimradi nipate pesa za kujikimu na familia yangu.''

'Sikutumia kinga kwa miezi kadhaa kwani wakati mwingi nilikuwa sina pesa za kununua mipira ya kondomu, na wateja wengine hawakutaka kutumia mipira hiyo," anasema Bi Felicia.

Image caption Bi Felicia katika Jumba la TRM

Bi Felicia alipata usaidizi kutoka kwa Shirika la Global Communication, ambalo huhudumu chini ya USAID ambalo huwasaidia wasichana kwenye mitaa ya mabanda jijini Nairobi kupata mafunzo anuwai kama vile ushauri nasaha, mbinu za mawasiliano,maadili mema na kuwatafutia nafasi za kazi.

Image caption Bi Felicia

Mkurugenzi wa mradi wa DREAMS bi Betty Adera amesema ni jukumu la mradi huo kuwanufaisha wasichana katika mitaaa ya mabanda jijini Nairobi kuishi maisha bora na kuwa kielelezo bora katika jamii.

''Bi Felicia ni miongoni mwa wasichana 200 tuliowachukua kutoka mtaa wa mabanda wa Majengo na kuwapa masomo ya kujiendeleza kimaisha.Baada ya wiki mbili, kupitia shirika letu la Global Communities,tuliungana na mmiliki wa biashara ya uoshaji magari na akawaajiri wasichana wanne miongoni mwao ni Felicia ambaye anafanya kazi ya uoshaji magari kwenye jumba la kibiashara la TRM kwenye barabara kuu ya Thika.'' Betty alisema.

Felicia amesema alikumbana na changamoto nyingi ikiwemo kutoka kwa wateja wakimuona kama msichana asiyeweza kufanya kazi inayodhaniwa kuwa ya wanaume pekee.

''Vifaa vya kazi vilikuwa vizito siku za kwanza, na bado sikuwa nimekubali ningeweza kufanya kazi hiyo ya uoshaji magari.''

Alikabiliwa pia na changamoto kubwa kutoka kwa wafanyikazi wengine, haswa wanaume, waliodhani anatishia kazi yao.

Kwa sasa Felicia ni muoshaji wa magari kwenye jumba la TRM, na anatumai kutimiza ndoto yake ya kuwa .......

Hii ni baada ya kufanyiwa mafunzo na kupata ushauri nahasa.

Anatumai kufanikisha ndoto yake ya kuwa mhasibu kutokana na mapato anoyoyapata kila siku kwa kazi hiyo ya uoshaji magari.