Rio 2016: Afisa ashtakiwa kwa kashfa ya fedha Kenya

Afisa mwengine wa Kenya akamatwa kwa tuhuma za kuhusika na kashfa ya kutoweka kwa mamilioni ya fedha Haki miliki ya picha AFP
Image caption Afisa mwengine wa Kenya akamatwa kwa tuhuma za kuhusika na kashfa ya kutoweka kwa mamilioni ya fedha

Afisa wa tano wa michezo ya Olimpiki nchini Kenya amekamatwa ikiwa ni miongoni mwa uchunguzi unaozunguka fedha na vifaa vilivyopotea katika mashindano ya Olimpiki mjini Rio.

Maafisa wa polisi walivamia nyumbani kwa Ben Ekumbo, ambaye ni makamu wa rais wa kamati ya Olimpiki na msimamizi wa shirikisho la waogeleaji.

Aliripotiwa kujificha chini ya kitanda.

Maafisa walipata maboksi ya viatu vya Nike pamoja na jezi ambazo zilikuwa hazijatumiwa ambazo zilipangwa kupewa wanariadha walioshiriki katika michezo hiyo.

Kukamatwa kwake kunajiri baada ya kudaiwa katika ripoti nyengine ya uchunguzi kwamba maafisa wakuu wa michezo waliiba zaidi ya pauni milioni 6.4 ,kama matumizi na vifaa vya wanariadha.

Maafisa wengine wanne walikamatwa mnamo mwezi Septemba.

Kiongozi wa ujumbe wa timu ya Kenya katika michezo hiyo Stephen Arap Soi alishtakiwa kwa kuiba dola milioni 250,000 ambazo zingetumika kugharamikia nauli,malazi pamoja na matumizi mengine ya wanariadha mjini Rio.

Makamu mwengine wa shirikisho hilo Pius Ochieng na katibu mkuu Francis Kinyili Paul pia walishtakiwa kwa kuiba jezi za Nike.