Uturuki yaondoa mswada wa ubakaji wa watoto kufuatia maandamano

Waandamanaji wanaopinga sheria inayowasamehe wanaume waliowabaka wasichana wadogo iwapo wamewaoa
Image caption Waandamanaji wanaopinga sheria inayowasamehe wanaume waliowabaka wasichana wadogo iwapo wamewaoa

Waziri mkuu wa Uturuki Binali Yildrim ameondoa mswada ambao unawasamehe wanaume waliowabaka wasichana wadogo iwapo wamewaoa.

Mswada huo ambao ulifanyiwa marekebisho ulirudishwa saa kadhaa kabla ya kupigiwa kura bungeni.

Ulikuwa umezua pingamizi katika jamii ya Uturuki na kushutumiwa ughaibuni.

Wakosoaji wanasema kuwa utahalalisha ubakaji na kuunga mkono mpango wa kuwaoa watoto wadogo.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yameitaka serikali kutoidhinisha mswada huo,wakihoji kwamba utaharibu uwezo wa taifa hilo kukabiliana na unyanyasaji wa kingono miongoni mwa watoto pamoja na ndoa za mapema.

Lakini serikali inasema kuwa lengo lake kuu ni kuwaondolea mashtaka wanaume wafungwa waliowaowa watoto wadogo kupitia ruhusa za familia zao.

Mswada huo utarudishwa katika tume ambayo itachukua maoni ya upinzani na mashirika ya kijamii,alisema bw. Yildirim.

Hii itaruhusu makubaliano na kutoa muda kwa upinzani kuwasilisha mapendekezo yake.