Wafuasi wa Trump wakerwa na uamuzi kuhusu Clinton

Hillary Clinton na Donald Trump. Haki miliki ya picha Getty Images

Wafuasi wahafidhina wa rais mteule wa Marekani Donald Trump wamelalamikia uamuzi wa kiongozi huyo wa kutofuatilia uchunguzi mpya kuhusu kashfa ya barua pepe iliyomkabili mpinzani wake Hillary Clinton.

Maafisa wake walitangaza Jumanne kwamba hatafuatilia ahadi yake ya kuhakikisha Bi Clinton anafungwa jela.

Bw Trump baadaye alifafanua na kusema hatua kama hiyo inaweza kuzua migawanyiko zaidi.

FBI walimuondolea Bi Clinton makosa lakini wafuasi wa Bw Trump walikuwa wakiimba "lock her up" (mfunge jela) kwenye mikutano yake ya kampeni.

Wafuasi wahafidhina sasa wanasema hatua hiyo ya Bw Trump ni "usaliti" na kwamba amevunja ahadi yake.

Tovuti ya Redstate.com imesema hatua ya Bw Trump kutomteua mwendesha mashtaka maalum wa kufuatilia tuhuma hizo dhidi ya Bi Clinton, kama alivyokuwa ameahidi, itafichua "ukweli kwamba yeye ni mtu aliyejidai kuwa wakati wa kampeni".

Tovuti ya mrengo wa kulia ya Breitbart News Network, moja ya tovuti za habari zinazomuunga mkono sana Bw Trump pia ilishutumu hatua hiyo na kusema ni "ahadi iliyovunjwa".Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Ann Coulter, ambaye ni mhafidhina, aliandika kwenye Twitter: "Whoa! Nilidhani tulimchagua @realDonaldTrump kuwa rais. Tulimfanya FBI, & DOJ? Kazi yake ni kuwateua, si kufanya kazi yao."

Kisha, alifuatiliza kwa ujumbe mwingine: "Hakuna rais anayefaa kuwa akiwazuia wachunguzi kufanya kazi yao. #EqualUnderLaw (Wote sawa mbele ya sheria)"

Shirika la kisheria linaloegemea sasa za mrengo wa kulia la Judicial Watch lilisema huo ni usaliti kwa Wamarekani kuhusu "ahadi yake kwa Wamarekani ya kuondoa maji yote kutoka kwa 'kinamasi' cha ufisadi uliokithiri Washington".

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wafuasi wa Bw Trump kwenye kampeni walifurahia ahadi yake ya kufunga Clinton

Wakati wa kampeni, Bw Trump alisema mpinzani wake alikuwa mtu mwovu sana na kuapa kwamba angehakikisha kesi zinafunguliwa dhidi yake.

Alimweleza kama mgombea mfisadi zaidi kuwahi kuwania urais nchini Marekani.

Lakini tangu uchaguzi kumalizika, alionekana kuanza kulegeza msimamo.

Wiki moja iliyopita, alisema familia ya Clinton ni ya "watu wema".

Kisha, Jumanne asubuhi, msemaji wake Kellyanne Conway alisema hakutakuwa na uchunguzi zaidi kuhusu barua pepe za Bi Clinton ili kumpa nafasi ya "kupona".

Saa chache baadaye, Bw Trump mwenyewe aliambia New York Times kwamba uchunguzi mpya haujafutiliwa kabisa lakini hakuna uwezekano mkubwa wa hilo kufanyika kwani litazua migawanyiko zaidi.

"Nataka kusonga mbele. Sitaki kurudi nyuma. Sitaku kuumiza familia ya Clinton, sitaki kamwe."

Kwenye mahojiano na New York Time, Bw Trump pia alijitenga na kundi la watu wanaotetea ubabe wa watu weupe (Wazungu) ambao walipiga saluti za Nazi wakisherehekea ushindi wake mjini Washington Jumamosi.

Pia, alisema:

  • Shemeji yake Jared Kushner, mfanyabiashara wa nyumba na makao ambaye hana ujuzi katika demokrasia, anaweza kusaidia kupatikana kwa amani kati ya Waisraeli na Wapalestina, alisema. Bw Kushner ni mumewe Ivanka, bintiye Bw Trump na ni Myahudi.
  • Marekani haifai kuwa "mjenzi wa mataifa" duniani, alisema.
  • Viongozi wa Republican Paul Ryan na Mitch McConnell "wanampenda tena, alisema
  • Anaweza kuendesha biashara zake na nchi pia, bila kuwa na mgongano wa maslahi
  • Kuna uhusiano fulani kati ya shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya tabia nchi

Bw Trump ataapishwa 20 Januari, 2017.


Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii