Foleni mbaya zaidi ya magari Los Angeles, Marekani

Huwezi kusikiliza tena
Msongamano mkubwa wa magari Los Angeles

Video ya foleni ndefu ya magari kusini mwa jimbo la California nchini Marekani imevuma sana mtandaoni, wengi wakisema huenda ndiyo foleni mbaya zaidi duniani.

Video hiyo ilipigwa kwa kutumia helikopta ya shirika la habari na inaonesha magari yakiwa yamekwama katika barabara nambari 405 katika mji wa Los Angeles Jumanne.

Wengi wa wakazi walikuwa wanakimbia nyumbani kuhudhuria sherehe za Siku ya Shukrani, moja ya siku zinazoenziwa sana Marekani.

"Haikuitwa 405 bure: inakuchukua saa 4 hadi 5 kufika popote," mtu mmoja aliandika kwenye Facebook.

Karibu watu 49 milioni wanatarajiwa kusafiri angalau maili 50 siku ya Alhamisi wakati wa sikukuu hiyo ambayo watu huisherehekea kwa kupatiana zawadi ya bata mzinga.

Idadi ya wanaosafiri mwaka huu ni milioni moja zaidi ya waliosafiri mwaka uliopita, na ndio wengi zaidi tangu 2007, kwa mujibu wa Chama cha Magari cha Marekani.

Baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii walisema foleni hiyo ndefu ya magari iliifanya barabara ya 405 kuonekana kana kwamba ilikuwa imepambwa kwa taa za Krismasi.

Sherehe ya Shukran ina asili yake karne ya 17 wakati Mahujaji waliotoroka Uingereza na nchi nyingine za Ulaya walipotua Plymouth, Massachusetts.

Walikuwa wanasherehekea mlo wa kwanza wa msimu pamoja na Wamarekani asili.

Mada zinazohusiana