Genge la ‘walaji rushwa’ lajitangaza gazetini Kenya

Tangazo lililochapishwa gazetini
Image caption Tangazo lililochapishwa gazetini

Wakenya wengi mtandaoni wameeleza kushangazwa kwao na tangazo lisilo la kawaida ambalo limechapishwa katika gazeti moja kuu nchini humo.

Tangazo hilo linawalenga watu wanaotaka kujiunga na „magenge ya ufisadi na kufaidi kwa kandarasi za kuiuzia serikali bidhaa na huduma bila kutoa jasho".

Aliyeweka tangazo hilo gazetini, kwenye sehemu ya matangazo ya biashara ya jumla, ameweka hata nambari ya simu.

Mwandishi wa BBC alipiga nambari hiyo ya simu na ikapokelewa na mwanamume ambaye alijitambulisha kama Master.

Anasema wanaotaka kufaidi wanafaa kuwa wamesajili kampuni rasmi na wawasilishe maelezo kwa „genge hilo".

Haki miliki ya picha TWITTER

Baada ya hapo, watafaidi kwa kandarasi na zabuni za serikali kupitia usaidizi wa genge hilo, ambalo alisema jina lake ni Shadow Cartel.

Katika jambo linaloashiria kwamba huenda ni matapeli tu, ili kujiunga na kundi hilo, Master alisema mtu atahitajika kulipa dola 500 za Kimarekani.

Anasema baada ya kushinda zabuni, mnufaika atahitaji kulipa asilimia 5 ya jumla ya thamani ya zabuni hiyo kwa genge hilo.

Haki miliki ya picha TWITTER

Mapema mwaka huu, aliyekuwa wakati huo Jaji Mkuu Dkt Willy Mutunga, ambaye kwa sasa amestaafu, alisema kwenye mahojiano na gazeti la NRC Handelsblad la Uholanzi kwamba Kenya ni taifa la "wanyang'anyi".

Alisema kwamba wananchi wanapigana vita na magenge ya watu sawa na 'mafia' ambayo yanaongozwa na viongozi wa kisiasa na wafanyabiashara wafisadi.

Aidha, alieleza kuwa Kenya ni ngome ya wahalifu wa magenge sawa na makundi ya Al Capone ya miaka ya 1920 nchini Marekani ambayo "yanajizolea mamilioni ya pesa kila siku" na kwamba ufisadi umekita mizizi kutoka ngazi ya chini ya taifa hadi kileleni.

Mada zinazohusiana