Magufuli afutilia mbali bodi ya TRA nchini Tanzania

Magufuli Haki miliki ya picha Facebook
Image caption Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli

Rais wa Tanzania ametangaza kwamba ameamua kumfuta kazi mwenyekiti wa Mamlaka ya Mapato nchini humo (TRA) na kuvunja bodi nzima baada ya uamuzi wao wa kuwekeza karibu dola milioni 13 katika akaunti za benki, gazeti la Daily News limeripoti.

Gazeti hilo limemkuu Dkt Magufuli akisema:

''Kumekuwa na uzoefu wa maafisa wa umma kuwekeza fedha za umma kwenye akaunti za benki na kutoweka na faida zinapopatikana kutokana na fedha hizo. Mfumo huo husababisha serikali kupata upungufu wa fedha na kusababisha watu kuomba mikopo katika benki na kulipa kwa kiwango kikubwa''

Pesa hizo zilikuwa katika bajeti ya shirika la mamlaka ya mapato, badala yake pesa hizo zilielekezwa kwenye benki na bodi hiyo ya TRA,rais aliongezea.

Baada ya kugundua hitilafu hiyo, nilitoa uamuzi kwamba pesa hizo zinastahili kurudishwa na bodi hiyo kufutiliwa mbali, Dkt Magufuli alielezea siku ya Alhamisi katika hotuba yake aliyoitoa katika chuo kikuu cha Open nchini Tanzania.