Mamilioni wasiofaa kupiga kura walipiga, Trump asema

Donald Trump Oktoba 016 Haki miliki ya picha AFP/Getty Images
Image caption Donald Trump hajatoa ushahidi wowote kuthibitisha madai yake

Rais Mteule Donald Trump amesema alishinda kwa wingi wa kura za kawaida "iwapo utaondoa kura za mamilioni ya watu ambao hawakufaa kupiga kura lakini walipiga".

Hata hivyo, hakutoa ushahidi wa kuthibitisha madai hayo yake.

Mwanachama huyo wa Republican, alishinda uchaguzi kwa kura za wajumbe, ambazo ndizo huamua mshindi wa urais Marekani.

Amesema hayo baada ya kambi ya mpinzani wake kutoka chama cha Democratic Hillary Clinton kutangaza kwamba wataunga mkono juhudi za kutaka kura zihesabiwe upya jimbo la Wisconsin.

Juhudi hizo zilianzishwa na mgombea wa chama cha Green, Jill Stein.

Bi Clinton alipata takriban kura 2 milioni za kawaida dhidi ya Bw Trump.

Hata hivyo, Bw Trump alipita kura 270 za wajumbe zinazohitajika kushinda urais.

Aliandika kwenye Twitter :"Licha ya kushinda Kura za Wajumbe pakubwa, pia nilishinda kura za kawaida ukiondoa kura za watu ambao hawakufaa kupiga kura lakini walipiga."

Haki miliki ya picha Twitter

Kwenye ujumbe wa kufuatiliza, aliandika: "Ingekuwa rahisi zaidi kwangu kushinda kura za kawaida kuliko Kura za Wajumbe kwa sababu ningehitajika kufanya kampeni katika majimbo 3 au 4 badala ya majimbo 15 ambayo nilitembelea.

"Ningeshinda kwa urahisi hata zaidi na kwa njia ya kuridhisha (lakini majimbo madogo yanasahaulika)!"

Bw Trump pia alidai kulitokea "ulaghai mwingi katika upigaji kura" majimbo ya Virginia, New Hampshire na California ambapo Bi Clinton alishinda.

Aliwashutumu wanahabari Marekani akisema wamekataa kuangazia suala hilo.

Awali mnamo Jumapili, rais huyo mteule alimkumbusha mpinzani wake wa chama cha Democratic Hillary Clinton kwamba alikuwa tayari amekubali kushindwa, na akachapisha maneno yake kutoka kwa midahalo ya urais ambapo alihimiza kukubaliwa kwa matokeo ya uchaguzi.

Wakati huo, Bi Clinton alikuwa akizungumzia hatua ya Bw Trump kukataa kuahidi kwamba angekubali matokeo ya uchaguzi wa urais iwapo angeshindwa.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Hillary Clinton alikubali kushindwa uchaguzi huo wa 8 Novemba

Bw Trump alimshinda Bi Clinton kwa kura chache katika jimbo la Wisconsin, ambapo mgombea wa chama cha Green Jill Stein aliitisha kuhesabiwa upya kwa kura wiki iliyopita.

Dkt Stein pia anataka kura zihesabiwe tena majimbo ya Michigan na Pennsylvania, akisema kuna "kasoro nyingi za kitakwimu".

Mgombea huyo anasema anataka kuhakikisha wadukuzi wa mifumo ya kompyuta hawakuingilia uchaguzi huo na kumsaidia Bw Trump.

Kabla ya uchaguzi, kulikuwepo na wasiwasi kutoka kwa baadhi kwamba huenda wadukuzi kutoka Urusi wangeingilia uchaguzi huo.

Serikali ya Marekani imesema mawakala wa serikali ya Urusi walihusika kudukua habari za Kamati ya Taifa ya chama cha Democratic, madai ambayo Urusi imeyakanusha.

Ili kubadili matokeo ya uchaguzi, itahitaji matokeo yabatilishwe katika majimbo ya Wisconsin, Michigan na Pennsylvania, jambo ambalo wachanganuzi wanasema ni ngumu mno.

Maafisa wa kampeni wa Bi Clinton walisema watashiriki shughuli ya kuhesabu upya kura jimbo la Wisconsin.

Mshauri mkuu wa kampeni Marc Elias alisema hakuna ushahidi kwamba uchaguzi huo uliingiliwa, lakini "tuna wajibu kwa Wamarekani 64 milioni waliompigia kura Hillary Clinton kushiriki katika shughuli hii inayoendelea kuhakikisha matokeo yanayripotiwa ni sahihi."

Jill Stein, 66, ni daktari na mwanaharakati ambaye alitarajia kupata uungwaji mkono kutoka kwa wafuasi wa Democratic waliomuunga mkono Bernie Sanders ambao walikuwa bado wanampinga Bi Clinton uchaguzini.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii