Maandamano India kupinga marufuku ya noti

Maandamano Delhi Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Maandamano dhidi ya marufuku ya noti hizo yamefanyika mji mkuu Delhi

Maelfu ya watu nchini India wameandamana kupinga hatua ya serikali ya kupiga marufuku noti za rupia 500 na 1,000 nchini humo.

Marufuku hiyo ilianza kutekelezwa usiku.

Maelfu ya watu wameendelea kupiga foleni katika benki wakitaka kusalimisha noti hizo zilizopigwa marufuku na kupata noti mpya.

Waziri Mkuu Narendra Modi ametetea uamuzi huo akisema hatua hiyo itasaidia kukabiliana na ulaji rushwa.

Lakini vyama vya upinzani vinasema mchakato huo uliendeshwa kwa njia isiyofaa.

Wiki iliyopita, upinzani ulikwamisha shughuli bungeni na kumtaka Bw Modi kuomba radhi kwa sababu ya hatua hiyo.

Waandishi wa habari wanasema haiwezekani kukadiria ni watu wangapi watakaojitokeza kuandamana kwani kunao baadhi ya raia wanaounga mkono marufuku hiyo.

Mawaziri wakuu wa majimbo ya Bihar na Orissa wamekataa kuunga mkono maandamano hayo wakisema juhudi za Bw Modi za kukabiliana na ufisadi zinafaa kuungwa mkono.

Maandamano yamefanyika katika miji ya Lucknow, Kolkata, na Bangalore.

Katika majimbo ya Kerala na Kerala, yanayotawaliwa na Wakomunisti, kuna uwezekano wa shughuli kukwama kabisa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Huduma za treni zimevurugwa katika jimbo la Tripura kaskazini mashariki mwa India

Takriban 90% ya shughuli zote za kibiashara hufanywa kwa pesa taslimu na watu wengi huwa hawana akaunti benki.

Noti zilizopigwa marufuku zilijumuisha 86% ya pesa zilizokuwa zinatumiwa katika uchumi wa nchi hiyo.

Akitoa hotuba yake ya kwanza ya kitaifa kuhusu marufuku hiyo Jumapili, Bw Modi aliwahimiza raia watumie sana mifumo ya dijitali kulipia huduma na bidhaa na wapunguze matumizi yao ya pesa taslimu.

Mada zinazohusiana