Luteni Seyoboka afikishwa mahakamani Rwanda

Mshukiwa wa mauaji ya kimbari Luteni Jean Claude Seyoboka
Image caption Mshukiwa wa mauaji ya kimbari Luteni Jean Claude Seyoboka

Mshukiwa wa mauaji ya kimbari Luteni Jean Claude Seyoboka aliyepelekwa Rwanda na nchi ya Canada kwa mara ya kwanza amefikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi kusomewa mashitaka dhidi yake.

Mahakama hiyo inataraji kutangaza ikiwa atashitakiwa akiwa gerezani au nje.

Luteni huyo alifikishwa mahakamani akiwa amevalia nguo zenye rangi ya kijani zinazotambulisha wafungwa wa kijeshi, ikiwa ni kwa mara ya kwanza kufikishwa mbele ya jaji, siku kumi baada ya kukabidhiwa Rwanda na mahakama ya Canada.

Baada ya kujibu maswali kuhusu wasifu wake, Luteni Seyoboka ameiambia mahakama kuwa hawezi kwendelea kuzungumza zaidi bila kuwepo kwa wakili wake, akisisitiza hajui lolote kuhusu sheria.

Wakili wake hakujitokeza mahakamani kwa sababu ambazo hata mahakama haikujua.

Kwa mjibu wa sheria, wakili anapokosekana kesi inaahirishwa hadi siku tatu.

Luteni Jean Claude Seyoboka mwenye umri wa miaka 50 alikuwa afisa wa jeshi la zamani chini ya utawala wa hayati Juvenal Habyarimana katika kikosi cha wanamizinga.

Baada ya mauaji ya kimbari alikimbilia nchini Canada .

Alifukuzwa na Canada ikimshtumu udanganyifu alipoomba hifafdhi.

Kadhalika Rwanda ilikuwa imetoa waranti ya kimataifa ya kumkamata.

Rwanda inamshtaki kuhusika kwa kupanga na kutekeleza mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Pamoja na hayo, mwaka 2007,mshukiwa huyo alihukumiwa bila kuwepo kifungo cha miaka 19 jela na mahakama za jadi nchini Rwanda maarufu Gacaca.

Hajatangaza kunaka ama kukubali mashtaka dhidi yake.

Huyu ni mshukiwa wa pili wa mauaji ya kimbari kukabidhiwa Rwanda na nchi ya Canada baada ya Leo Mugesera miaka 4 iliyopita na ambaye mwaka jana alihukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya kimbari.