Mshambuliaji wa Ohio Abdul Ali Artan ni 'mkimbizi kutoka Somalia'

Polisi wanasema mwanamume huyo alivurumisha gari hadi kwenye umati wa watu Haki miliki ya picha AP
Image caption Polisi wanasema mwanamume huyo alivurumisha gari hadi kwenye umati wa watu

Mwanamume aliyewashambulia na kuwajeruhi watu 11 katia Chuo Kikuu cha Ohio ni asili a Kisomali na alikuwa mwanafunzi katika chuo hicho, maafisa nchini Marekani wanasema.

Abdul Razak Ali Artan, 18, alivurumisha gari hadi kwenye kundi la watu waliokuwa wakipita chuoni na kisha akatoka nje na kuanza kuwadunga kwa kisu.

Alipigwa risasi na kuuawa na maafisa wa polisi.

Mkuu wa polisi wa eneo hilo Kim Jacobs amesema wanachunguza kubaini iwapo shambulio hilo lililotokea Jumatatu asubuhi lilikuwa la kigaidi.

FBI pia wanashiriki katika uchunguzi huo.

Shambulio hilo lilitokea katika bewa la chuo kikuu hicho mjini Colombus ambalo huwa na wanafunzi takriban 60,000.

Artan alikuwa mhamiaji kutoka Somalia ambaye amekuwa akiishi Marekani kama mkazi wa kudumu kwa njia halali, vyombo vya habari Marekani vimeripoti.

Alipoulizwa kwenye kikao na wanahabari iwapo hilo lilikuwa shambulio la kigaidi, mkuu wa polisi Bw Jacobs alisema: "Nafikiri tunahitaji kuchunguza hilo."

Kisha, akaongeza: "Bila shaka, ukizingatia nia ambayo ilionekana wazi, kuendesha gari kwenye njia inayotumiwa na watu kutembea, tunachunguza kubaini iwapo ni kisa kilichokuwa kimepangwa."

Haki miliki ya picha ABC
Image caption Wanafunzi wakiwa wameziba mlango wa moja ya madarasa katika chuo cha Ohio

Artan alisomea somo la usimamizi wa mipango katika kitivo cha Biashara katika chuo hicho, gazeti la Columbus Dispatch limeripoti.

Kisa kilianza mwendo wa saa nne asubuhi Jumatatu pale gari liliporuka na kuanza kuwagonga wapita nia karibu na ukumbi wa Watts Hall.

Baadaye, dereva wa gari hilo alitoka nje na kuanza kuwadunga kisu watu.

Afisa wa polisi Alan Horujko, 28, aliyekuwa karibu alimpiga risasi na kumuua katika kipindi cha chini ya dakika moja.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Chuo Kikuu cha Jimbo la Ohio ni moja ya vyuo vikuu vikubwa zaidi Marekani
Haki miliki ya picha AP
Image caption Baada ya shughuli kusitishwa kwa muda, wanafunzi walikaguliwa na polisi na kuruhusiwa kuondoka chuoni

Mada zinazohusiana