Trump amteua mkosoaji wa Obamacare Tom Price kuwa waziri

Tom Price Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Tom Price ateuliwa kuwa waziri wa afya

Rais mteule wa Marekani Donald Trump amemteua Tom Price kuwa waziri wa Afya katika serikali yake.

Bw Price, 62,amekuwa katika Bunge la Congress akiwakilisha jimbo la Georgia na ni mtaalam wa upasuaji wa mifupa ambaye amekuwa akiongoza kamati ya bajeti katika Bunge la Wawakilishi.

Atatekeleza jukumu muhimu katika mipango ya chama cha Republican wa kubatilisha mpango wa bima ya afya ulioanzishwa na Rais Obama, ambao hufahamika sana kama Obamacare.

Wakati wa kampeni Bw Trump aliapa kwamba ataibatilisha sheria hiyo ambayo imekuwa ikitazamwa kama moja ya mambo makuu aliyoyafanya Bw Obama wakati wa utawala wake.

Lakini amesema kwamba kuna baadhi ya vipengele vya sheria hiyo ambavyo atavihifadhi.