Trump: Aliyeshambulia Ohio hakufaa kuingia Marekani

Mshambuliaji wa chuo kikuu cha Ohio Abdul Razak Ali kulia
Image caption Mshambuliaji wa chuo kikuu cha Ohio Abdul Razak Ali kulia

Rais mteule wa Marekani Donald Trump amesema kuwa mkimbizi wa Kisomali aliyetekeleza mashambulizi katika chuo kikuu cha Ohio siku ya Jumatatu hangefaa kuruhusiwa kuingia nchini humo.

Trump amesema kuwa wapiganaji wa ISIS wanajilimbikizia sifa kwa shambulio hilo lililowaacha watu 11 wakiwa wamejeruhiwa.

Kitengo cha wapiganaji hao kimemtaja mwanafunzi huyo wa somo la biashara Abdul Razak Ali Artan kama ''mwanajeshi''.

Image caption Mshambuliaji wa Ohio

Mamake kijana huyo mwenye umri wa miaka 18 anasema kuwa mwanawe hakuonyesha ishara zozote za kutaka kutekeleza shambulio hilo katika chuo kikuu cha Ohio mjini Colombus.

Waziri wa maswala ya ndani Jeh Johnson alisema kuwa wachunguzi hawajapata uhusiano wowote kati ya Artan na kundi lolote la kigaidi.

Ajenti maalum wa shirika la ujasusi FBI Angela Byers alisema kwamba Artan huenda alishawishiwa na kiongozi wa Al-Qaeda Anwar al-Awlaki ambaye aliuawa na shambulio la ndege zisizo na rubani nchini Yemen mwaka 2011.

Image caption Polisi aliyemuua mshambuliaji wa chuo kikuu cha Ohio

Artan alikuwa mkimbizi ambaye alihama na familia yake 2014 kuelekea Marekani kutoka Pakistan ambapo amekuwa akiishi tangu 2007.