Mgomo wakwamisha huduma ya afya Kenya

Wanataka serikali kutekeleza muafaka wa 2015 wa utenda kazi Haki miliki ya picha AP
Image caption Madaktari wameapa kutorejea kazini hadi mazingira yaboreshwe

Maelfu ya wagonjwa katika hospitali za umma nchini Kenya wanahangaika bila matibabu kufuatia mgomo wa kitaifa wa madaktari na wahudumu wengine wa afya.

Mgomo huu umeanza wiki hii ambapo madaktari wanashinikiza serikali kutekeleza muafaka wa mwaka 2013 iliyoafikiwa na muungano wa wahudumu wa afya, kuboresha mazingira ya kazi.

Hii ni pamoja na nyongeza ya marupurupu na kuweka vifaa na dawa hospitalini.

Taarifa za vyombo vya habari nchini Kenya zinasema karibu wagonjwa 100 wametoroka kutoka hospitali kuu inayoshughulikia matatizo ya akili ya Mathari mjini Nairobi . Polisi wanasema wamefanikiwa kuwarejesha baadhi yao hospitalini.

Wagonjwa wengine katika hospitali za umma nchini wamelazimika kurudi nyumbani au kutafuta matibabu katika vituo binafsi ambavyo gharama yake ni juu.

Mwaka wa 2013, sekta ya afya nchini Kenya ilipeleka baadhi ya huduma zake chini ya mamlaka za Kaunti.

Hatua hiyo ilipelekea hospitali za umma kuwa chini ya usimamizi wa magavana.Hata hivyo Wizara ya afya bado inasimamia hospitali kuu za kitaifa ile ya Kenyatta iliyoko mjini Nairobi na Moi iliyoko Magharibi mwa Kenya.

Image caption Wagonjwa wengi hawana wa kuwahudumia

Tangu sekta ya afya kuwekwa chini ya usimamizi wa kaunti, huduma ya afya imeonekana kudorora huku wauguzi na madaktari wakifanya migomo ya kila mara kulalamikia mazingira duni ya kazi.

Mvutano kati ya serikali kuu na Kaunti kuhusu utoaji wa vifaa muhimu katika vituo vya afya pia imeyumbisha sekta ya afya nchini Kenya.

Wizara ya afya imekua ikiwasihi wahudumu wa afya kutogoma ili kuokoa maisha ya wagonjwa, na kuwapa muda kutathmini muafaka huo,lakini ombi lao limeonekana kupuuzwa.

Hakuna taarifa imetolewa na wizara ya afya kuhusu hali ya sasa katika hospitali za umma, huku baadhi ya magavana wakitishia kuwafuta kazi wote watakaoshiriki kwenye mgomo.