Twiga wamo hatarini ya kuangamia

Twiga Haki miliki ya picha IUCN
Image caption Idadi ya twiga imepungua sana maeneo mengi Afrika

Twiga wamepungua sana duniani katika kipindi cha miaka 30 iliyopita na kwa sasa wanakabiliwa na hatari ya kuangamia.

Idadi ya twiga duniani imeshuka kutoka 155,000 mwaka 1985 hadi 97,000 mwaka 2015 kwa mujibu wa shirika la kimataifa la uhifadhi wa mambo asilia (IUCN).

Idadi ya wanyama hao imepungua sana kutokana na kuharibiwa kwa maeneo wanamoishi, uwindaji haramu na migogoro ya kisiasa katika maeneo mengi Afrika.

Baadhi ya aina wa twiga, sana maeneo ya kusini ya Afrika, wanaongezeka hata hivyo.

Hadi kufikia sasa, IUCN hawakuwa wameorodhesha twiga kuwa miongoni mwa wanyama walio hatarini.

Hata hivyo, kwenye orodha yao mpya ya wanyama walio hatarini, mnyama huyo ameorodheshwa kuwa "hatarini", baada ya idadi ya wanyama hao kushuka kwa zaidi ya asilimia 30.

Kwa mujibu wa Dkt Julian Fennessy, mwenyekiti wa kundi la IUCN linaloshughulikia twiga, wanyama hao "wanaangamia kimya kimya."

"Ukienda kwenye safari, twiga wapo kila mahali," aliambia BBC News.

"Ingawa kumekuwepo na wasiwasi kuhusu ndovu na vifaru, twiga wamesahaulika. Ni jambo la kusikitisha kwamba idadi yao imeshuka sana na ni jambo la kushangaza, kwamba wamepungua hivyo katika kipindi kifupi."

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Twiga hupenda sana kupeleleza na hili huwafanya kuwindwa kwa urahisi na majangili na wapiganaji

Ongezeko kubwa la idadi ya watu limesababisha maeneo mengi ya misitu kuharibiwa kwa ajili ya kilimo, jambo ambalo limepunguza maeneo wanamoishi twiga.

Vita katika baadhi ya maeneo Afrika pia vimeathiri idadi yao.

"Katika maeneo haya yenye vita na migogoro, hasa kaskazini mwa Kenya, Somalia na Ethiopia katika mpaka wake na Sudan Kusini, twiga ambao ni wanyama wakubwa wanaliwa."

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii