Watu 1.2m kuhudhuria sherehe ya kuzaliwa Mexico

Crescencio Ibarra na mkewe walikusudia kualika majirani na marafiki pekee Haki miliki ya picha Facebook
Image caption Crescencio Ibarra na mkewe walikusudia kualika majirani na marafiki pekee

Watu zaidi ya milioni moja wamesema watahudhuria sherehe ya kuzaliwa ya msichana mmoja nchini Mexico baada ya mwaliko uliotolewa na babake kuvuma sana mtandaoni.

Polisi watatumwa katika kijiji anamotoka msichana huyo kudhibiti watu.

Kwenye video ya kuwaalika watu, babake msichana huyo alikuwa amesema "kila mtu anaalikwa" kwenye sherehe hiyo ambayo itakuwa na muziki wa bendi, chakula na mbio za farasi.

Alipakia video hiyo kwenye Facebook ikiwa wazi kwa wote.

Anasema lengo lake lilikuwa kuwaalika majirani na marafiki pekee. Lakini anasema wote watakaofika, hatawafukuza.

Video hiyo inamuonyesha Bw Crescencio Ibarra akiwa amesimama na bintiye Rubi, aliyevalia taji kichwani, pamoja na mkewe Anaelda Garcia.

"Hujambo, hali yako ikoje? Tunakwalika tarehe 26 Desemba uhudhurie sherehe ya kuzaliwa ya 15 ya binti wetu, Rubi Ibarra Garcia," Bw Ibarra, anasema huku bintiye akitabasamu.

Baadaye, anataja bendi tatu ambazo zitatumbuiza na kwamba mshindi wa mbio za farasi atatuzwa peso 10,000 ($490; £390).

Haki miliki ya picha Twitter
Image caption Baadhi wameunda kadi bandia za mwaliko, zikiwa na majina ya bendi zitakazotumbuiza

Anamaliza kwa kusema "kila mtu anaalikwa, kwa moyo mkunjufu".

Sherehe ya kuzaliwa ya 15 huwa ni hafla kubwa na muhimu sana Mexico, kwani hutazamwa kama wakati ambao msichana amekomaa.

Msichana hupambwa kama "malkia wa siku".

Haijabainika ni kwa nini video hiyo ilivuma sana na kusambazwa zaidi ya mara 800,000 mtandaoni, na hata watu wengi kuanzisha utani katika mitandao ya kijamii.

San Luis Potosi

Haki miliki ya picha Twitter
Image caption Baadhi ya kampuni zimetumia fursa hiyo kujitangaza, mfano shirika la ndege la Interjet linalouliza watu: "Je, unahudhuria sherehe ya kuzaliwa ya 15 ya Rubi?" na kuahidi kipunguzo cha 30% kwenye nauli kwenda mji anamotoka Rubi, San Luis Potosi
Haki miliki ya picha El Show de Piolin
Image caption Mwigizaji wa Mexico Gael Garcia Bernal (kushoto) amemuigiza Bw Ibarra kwenye kipindi chake cha ucheshi.