Mesut Ozil kuuzwa asiposaini mkataba

Ujerumani
Image caption Mesut Ozil kiungo wa kimataifa wa Ujerumani

Klabu ya Arsenal inadaiwa kuwa tayari kusikiliza ofa kwa kiungo wa kimataifa wa Ujerumani Mesut Ozil kama asipokubali kusaini mkataba mpya.

Mkataba wa sasa wa nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 unamalizika kiangazi mwaka 2018, lakini meneja wa Arsenal, Arsene Wenger anaweza kumuuza kabla kama asipoongeza mkataba wake.

Wote wawili Alexis Sanchez na Ozil mikataba yao inamalizika sawa na wamekuwa wakihusishwa na tetesi za kuondoka Emirates.

Hata hivyo, Wenger anadaiwa kutotaka mkataba wa Ozil uishe na anaweza kuamua kumuuza huku Chelsea, Manchester City na Juventus zikidaiwa kumtaka.

Uhamisho kwenda Real Madrid pia unatajwa, kufuatia mwenyewe kueleza huko nyuma kuwa yuko tayari kurejea Santiago Bernabeu.