Waliomlazimisha mwafrika kuingia jeneza wanyimwa dhamana Afrika Kusini

Video ilimuonyesha mwanamme mzungu akimlazimisha mwanamme mwafrika kuingia kwenye jeneza Haki miliki ya picha YOUTUBE
Image caption Video ilimuonyesha mwanamme mzungu akimlazimisha mwanamme mwafrika kuingia kwenye jeneza

Wakulima wawili wazungu nchini Afrika kusini wanaolaumiwa kwa kumlazimisha mwanamme mwafrika kuingia kwenye jeneza kwa kupitita shamba lao wamenyimwa dhamana na mahakama.

Mwezi uliopita Theo Martins Jackson na Willem Oosthuizen, walifunguliwa mashtaka ya kuteka nyara na kudhuluma kwa viwango vya kusababisha madhara ya kimwili.

Walikamatwa baada ya video moja ya dakika ishirini ambayo ilirekodiwa tarehe 17 mwezi Agosti kuanza kusambaa mitandaoni ikionyesha mwanamme mzungu akimlazimisha mwanamme mwafrika kuingia kwenye jeneza, akimtishia kumumwagia mafuta na kumchoma.

Taarifa zinasema kuwa mwendesha mashtaka alipinga wawili hao kuachuliwa kwa dhamana akidai kuwa muathiriwa Victor Mlotshwa ametishiwa maisha tangu akamatwe.

Jaji anayesikiliza kesi ametaja kitendo hicho kuwa cha kushangaza na cha kibaguzi na kuongeza kuwa si jambo la kushangaza kuwa ulimwengi ulishtushwa nacho.