Afrika kusini yataka ufafanuzi kutoka ICC kuhusu kesi ya Bashir

Bashir Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Rais wa Sudan Omar el Bashir

Waziri wa haki wa Afrika kusini, Michael Masutha, amesema serikali imeiandikia mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC, ikiitaka kutoa ufafanuzi kuhusu kesi ya rais wa Sudan Omar al Bashir.

Hii ni baada ya mahakama ya ICC kusema kuwa, itafanya mkutano wa hadhara mwaka ujao mwezi Aprili ili kudadisi iwapo Afrika kusini, ilikosa kutimiza agizo la kumkamata rais Bashir mwaka jana.

Mahakama hiyo ya ICC imeitaka Afrika Kusini kutuma waakilishi wake kuisikiliza kesi hiyo mwaka ujao ili kujieleza ni kwa nini hawakutekeleza agizo la ICC la kukamata Bw Bashir alipokuwa nchini humo.

Bw Bashir alikuwa mjini Johannesburg kuhudhuria mkutano wa AU mwezi Juni mwaka jana

Lakini aliondoka nchini humo licha ya agizo la kumtaka kuzuiliwa asiondoke nchini humo.

Mahakama ya Pretoria iliamua iwapo itamkamata kulingana na agizo lililotolewa na ICC.

Mahakama kuu ya Pretoria ilitoa agizo la bw Bashir kukamatwa saa chache baada ya ndege yake kuondoka nchini humo na baadaye jaji wa mahakama hiyo aliishutumu serikali kwa kumruhusu rais huyo kuondoka .

Afrika kusini imetangaza kujiondoa kutoka kwa mahakama hiyo ya ICC, huku waziri huyo akisema haikutaka kutekeleza amri ya mahakama ya ICC ambayo ingesababisha ''mabadiliko serikaini.''

Bw Bashir anatafutwa na mahakama ya ICC kwa mashtaka ya mauaji ya halaiki na mashtaka ya uhalifu.

Bashir amekana madai kwamba alitekeleza mauaji magharibi mwa darfur nchini sudan