Rais Magufuli akutana na Dangote

Aliko Dangote
Image caption Aliko Dangote

Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amefanya mazungumzo na mmiliki wa kiwanda cha Saruji cha Dangote, Alhaji Aliko Dangote.

Katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli amemhakikishia mfanyabiashara huyo kuwa serikali ya Tanzania itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wote nchini kwa lengo la kuimarisha sekta ya viwanda nchini humo.

Aidha Magufuli amekanusha uvumi unaondelea kuhusu kiwanda cha kuzalisha Saruji cha Dangote akisema kuwa hakukuwepo na tatizo lolote ila watu waliotaka kujinufaisha binafsi kupitia mradi huo

Amemtaka Dangote kununua gesi moja kwa moja kutoka TPDC ambacho ni chombo cha serikali badala ya kutumia watu ambao wamekuwa na nia ya kutengeneza faida tu.

Image caption Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania

Kwa upande wake Dangote, ameshangazwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa amefunga kiwanda kwa sababu amekatazwa kuagiza makaa ya mawe kutoka nje ya Tanzania.

Dangote amesema kuwa makaa ya mawe ya Tanzania ni rahisi na yana ubora kuliko kuagiza nje.

Tayari Mfanyibiashara huyo ameingiza malori mapya 600 kwa ajili ya kusambazia saruji yake.