Majambazi waiba dhahabu ya kilo 70 Ufaransa

Magari Haki miliki ya picha AP
Image caption Polisi wakichunguza mabaki ya magari yaliyoteketea wakati wa kisa hicho karibu na mji wa Lyon

Majambazi waliokuwa na silaha wameiba dhahabu ya kilo 70 nchini Ufaransa na kutoroka.

Majambazi hao wanne waliokuwa wameabiri magari mawili walishambulia gari la usalama lililokuwa likisafirisha dhahabu hiyo karibu na mji wa Lyon.

Walitumia gari moja kuziba barabara.

Kisha, walichukua dhahabu hiyo inayokadiriwa kuwa ya thamani ya €1.5m ($1.6m; £1.3m), na kuipakia kwenye gari moja lao ambalo walikuwa wamepanga kulitumia kutoroka.

Baada ya hapo, waliwafungia walinzi wawili waliokuwa wanasafirisha dhahabu hiyo nyuma ya gari lao kabla ya kuteketeza gari ambalo walikuwa wamelitumia kufunga barabara.

Walinzi hao waliokolewa na maafisa wa polisi baada ya mtu aliyeshuhudia tukio hilo kuwapasha habari.

Wezi hao walitoroka upesi na kuacha moto uliokuwa kwenye gari waliloliwasha moto ukienea na kufikia magari mengine yaliyokuwa karibu ingawa muda mfupi baadaye wazima moto walifika na kuuzima.

Kisa hicho kilitokea katika barabara ya A6 inayounganisha Lyon na Paris.

Polisi wanawasaka wahusika.

Haki miliki ya picha Royal Mint
Image caption Vipande vya dhahabu

Visa vingine vikubwa vya wizi:

  • Oktoba, Kim Kardashian aliporwa na watu waliokuwa wamevalia kama maafisa wa polisi akiwa katika hoteli moja Paris. Polisi wanasema wezi hao waliiba vito vya takriban €6m.
  • Wanaume waliokuwa wamevalia barakoa waliwashambulia na kuwapora wanawake wawili kutoka Qatar wakiwa na dereva wao katika barabara moja kaskazini mwa Paris mwezi Novemba. Waliiba vito na mali nyingine, vyote vya thamani ya €5m.
  • Novemba, mwanamume mmoja alitoroka na ndoo iliyojaa dhahabu ya thamani ya $1.6m, baada ya mlango wa lori la kusafirisha dhahabu kuachwa ukiwa wazi bila kuwa na mtu aliyekuwa anauchunga.

Mada zinazohusiana