Donald Trump kuwakabidhi wanawe biashara zake

Donald Trump alizema mwezi uliopita kwamba hatajihusisha na biashara zake akiwa rais Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Donald Trump alizema mwezi uliopita kwamba hatajihusisha na biashara zake akiwa rais

Rais mteule wa Marekani Donald Trump amesema biashara zake zitasimamiwa na kuendeshwa na wanawe wawili atakapokuwa rais.

Wanawe hao ni Donald junior na Eric, ambao tayari wamekuwa wakitekeleza majukumu muhimu katika uendeshaji wa baadhi ya biashara.

Bw Trump amesema atawakabidhi biashara hizo kabla yake kuapishwa na kwamba hakuna mikataba mipya ya kibiashara ambayo itaingiwa na kampuni zake kipindi ambacho atakuwa anahudumu kama rais.

Wakosoaji wa rais huyo mteule wanasema bado atakuwa hatarini ya kutokea kwa mgongano wa maslahi iwapo hataachilia umiliki wa biashara zake.

Bintiye mkubwa Ivanka, ambaye amekuwa akijihusisha sana katika shughuli zake hajatajwa popote, jambo ambalo limewafanya badhi kufikiria labda atapewa kazi rasmi katika serikali ya Bw Trump.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Donald Trump Jr

Maafisa wa Trump wanaosimamia shughuli ya mpito wamesema kikao cha wanahabari ambacho kilitarajiwa wiki hii kuhusu nini itakuwa hatima ya kampuni zinazomilikiwa na Trump kimeahirishwa kwa muda usiojulikana kutoa muda wa kuandaliwa kwa mpango wa kina.

Msemaji wa Bw Trump amesema kikao hicho, ambacho kilitarajiwa kufanyika Alhamisi wiki hii, sasa kitafanyika Januari.

Hayo yakijiri, Bw Trump amesema atamteua rais wa Goldman Sachs Gary Cohn kuwa mshauri wake mkuu wa masuala ya kiuchumi.Bw Cohn atakuwa mkuu wa Baraza la Uchumi wa Taifa White House, wadhifa ambao utamfanya kuwa mmoja wa watu wenye usemi zaidi kuhusu maamuzi ya kiuchumi katika ikulu ya White House.

Image caption Maeneo ambayo Bw Trump ana biashara

Rais huyo wa Goldman ndiye mtu wa tatu kutoka kwenye benki hiyo kupewa wadhifa kwenye baraza la mawaziri la Bw Trump.

Steven Mnuchin, waziri mpya wa fedha, na Steve Bannon mshauri mkuu wa White House wote walikuwa maafisa watendaji katika benki ya Goldman.

Bw Trump pia amesema atatangaza uamuzi wake wa nani atakuwa waziri wa mambo ya nje katika serikali yake Jumanne asubuhi.

Maafisa wake wa mpito wamesema nafasi hiyo huenda ikapewa Rex Tillerson, afisa mkuu mtendaji wa Exxon Mobil.

Kuna wasiwasi kutokana na uhusiano wa karibu kati ya Bw Tillerson na rais wa Urusi Vladimir Putin.

Kama mkuu wa kampuni ya mafuta ya Exxon Mobil, amekuwa akikutana na kuzungumza na viongozi wengi wa kimataifa kuhusu mikataba ya kibiashara.

Mmoja wa waandishi wa BBC aliyepo Washington anasema akiteuliwa, hiyo itakuwa ishara nyingine kwamba Bw Trump anatazama sera za mambo ya nje kama biashara, ambapo atakuwa anamtuma waziri wake wa mambo ya nje kwenda kupata mikataba bora zaidi kwa Marekani katika ngazi ya kimataifa.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii